Mbinu za kukuepusha na saratani, kisukari

Thursday January 21 2021
mbinupic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Wakati takwimu zikionyesha Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wapya 50,000 wa saratani, wataalamu wameeleza kuwa kubadili mtindo wa maisha ndiyo mwarobaini wa kukabiliana na ugonjwa huo na mengine yasiyo ya kuambukiza.

Njia nyingine ni utamaduni wa kupima afya, kuzingatia lishe bora pamoja na kufanya mazoezi.

Juzi Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima alisema inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na ongezeko la asilimia 50 ya wagonjwa wapya wa saratani.

Ongezeko hilo ni kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na utafiti wa saratani (IARC).

Kwa mujibu wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), saratani zenye idadi kubwa ya wagonjwa kwa upande wa wanaume ni ile ya tezidume asilimia 23, koo la chakula asilimia 16, kichwa na shingo asilimia 12 na utumbo mkubwa na mdogo asilimia 11.4

Upande wa wanawake saratani inayoongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa ni shingo ya kizazi kwa asilimia 47, matiti asilimia 16, utumbo mkubwa na mdogo asilimia 5.8 na koo la chakula asilimia 5.3.

Advertisement

Dk Gwajima alisema magonjwa yasiyoambukiza kama saratani inashika nafasi ya tano kwa wanaume na ya pili kwa wanawake kwa kusababisha vifo vingi.

Mengine yanayosumbua ni kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, selimundu na magonjwa ya figo ambayo kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) yanachangia zaidi ya vifo milioni 41.

Kukabiliana nayo

Kukabiliana na hali hiyo, watalaam wameshauri kuzingatiwa mambo matatu ikiwa ni pamoja na utamaduni wa kupima afya, kuzingatia lishe bora pamoja na kufanya mazoezi.

Akizungumza na Mwananchi jana, daktari bingwa wa magonjwa ya vichocheo vya mwili, Wolfgang Benard alisema inaweza kumchukua mtu muda mrefu kujua kuwa ana ugonjwa wowote usiombukiza hivyo, ili kujua kama una tatizo lolote ni muhimu kufanya vipimo angalau mara mbili kwa mwaka.

Akitolea mfano wa ugonjwa wa kisukari, alisema idadi ya wanaojitambua kuwa wanaishi na ugonjwa huo ni ndogo ikilinganishwa na watu wasiojua.

“Watu wengi wanaishi na ugonjwa huu kwa muda mrefu bila kujua na upo uwezekano wasiojulikana kuwa na ugonjwa huu ndio wengi. Jinsi unavyokaa na ugonjwa huu kwa muda mrefu ndipo uwezekano wa kupata madhara unakuwa mkubwa,” alisema Dk Benard.

Hilo liligusiwa pia na Dk Gwajima kwa wagonjwa wa saratani akieleza kuwa asilimia 75 hufika katika vituo vya matibabu wakiwa wamechelewa sana na kuwawia vigumu madaktari kutibu na kuponya ugonjwa huo.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya tiba shufaa duniani, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa ORCI, Dk Mark Mseti alisema asilimia 70 hadi 80 ya wagonjwa hufika hospitalini hapo wakiwa hatua ya tatu na nne ambazo ni ngumu kutibika hivyo kuhitaji kupatiwa tiba shufaa.

“Ni asilimia 20 pekee ambao hufika ugonjwa ukiwa hatua ya kwanza na pili ambazo huweza kutibika, hawa asilimia 70 hadi 80 huhitaji tiba shufaa wakati tunaendelea na matibabu yao, hivyo utaona uhitaji wa huduma,’’ alisema.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na figo, Mazhar Amirali alieleza kuwa ulaji wa mboga za majani, matunda na vyakula visivyo na kufanya mazoezi husaidia kuziweka figo salama.

“Kwenye ulaji ni muhimu kuzingatia lishe yenye afya ikisisitza kupunguza ulaji wa vyakula vilivyosagwa, sukari, mafuta na nyama, chumvi kidogo hasa baada ya umri wa miaka 40 itasaidia kuzuia msukumo wa juu wa damu na kuwapo kwa mawe ya figo,”alisema na kuongeza kuwa mazoezi ya kila mara hudumisha msukumo wa kawaida wa damu na kudhibiti kisukari.

Shughuli za kimwili huondoa hatari ya kisukari, na msukumo wa juu wa damu hivyo basi kupunguza hatari ya ugonjwa sugu wa figo.
  

Advertisement