Mbowe adai kubambikwa kodi ya Sh2 bilioni, TRA yamtaka awapelekee malalamiko yake

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilimbambikizia kodi ya Sh2 bilioni na kufungia akaunti zake za benki jambo lililomfanya aamue kuondoka nchini na kwenda kuwekeza nchi zingine.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe ametaja sababu ya kuamua kuondoka nchini na kwenda kuwekeza nchi zingine kuwa ni tozo ya kodi kiasi cha Sh2 bilioni aliyopewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa kodi na mawasiliano, Richard Kayombo alipoulizwa kwa simu leo, amesema masuala ya kodi ni kati ya mlipa kodi na mamlaka hiyo, hivyo hatayazungumza kwenye vyombo vya habari.  


"Sipendi kuongea kwenye hilo kwa sababu suala la mlipa kodi anawasiliana na sisi moja kwa moja. Mlipakodi kama ana concern (jambo) anayo haki ya kuwasilisha lalamiko lake katika ngazi mbali mbali za Mamlaka au katika vyombo vya usuluhishi wa migogoro ya kodi,” amesema Kayombo. 


Mbowe ameyasema hayo leo Jumapili Aprili 11, 2021 wakati akilihutubia Taifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, akidai kuwa kabla ya kupewa tozo hiyo aliondolewa dhamana katika kesi yake ya uchaguzi na kuwekwa ndani miezi minne na kipindi hicho TRA walimtumia barua pepe kuelezea deni hilo la kodi wakijua fika hakuwa katika nafasi ya kupata ujumbe huo.


“TRA ilisema ninadaiwa kodi ya takribani bilioni mbili kitu ambacho si kweli hakuna deni hilo. Unapoidai kampuni kodi hiyo ina maana inatengeneza faida kwa mwaka bilioni 12 kwa hiyo faida yake itakuwa bilioni 50, hii ni kampuni yangu ndogo ya kifamilia haiwezi kutengeneza hiyo fedha hata kwa miaka 20,” amesema Mbowe.


Mbowe amesema yote hayo yalifanyika wakijua yupo gerezani hawezi kupokea barua pepe, “walifahamu fika haitanifikia baada ya siku 60 wakaandika kwamba tulikuandikia barua wakafungia akaunti zangu.”


Mbowe amesema kilichomshangaza mapema wiki jana TRA wamemwandikia barua kuwa wamefungua akaunti zake.
“Nimepokea barua kuwa zile akaunti zako, zuio la akaunti tunafungua hamnimbii fedha mlizochukua ni kiasi gani? Udhalilisaji mlionifanyia, usumbufu mlionisababishia, uhuni mlionifanyia na ni Watanzania wangapi walifanyiwa haya?” Amehoji Mbowe.


Baada ya kauli hiyo amesema hiyo ndiyo sababu mojawapo iliyomfanya aondoke nchini kwenda kuwekeza nchi zingine.
 “Kila biashara niliyojitahidi kuifanya ilivunjwa, ilifungwa, ilibomolewa, nilienda nje kwa sababu Serikali ya Magufuli na watu wake hawakutaka nifanye biashara, sawa mtanifungia Tanzania hamtanifungia Afrika Kusini, Marekani, Dubai au nchi nyingine.


“Huyu ni Mbowe alifanyiwa haya kwa sababu ni Mwenyekiti wa Chadema je? Ni Watanzania wangapi wa asili mbalimbali wenye uwekezaji hapa ambao wamekimbia taifa hili na kuhamisha mitaji?” Amehoji.