Mbowe amkumbusha Samia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa

Wednesday June 09 2021
chademapic

Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) Taifa Freeman Mbowe

By Mwandishi Wetu

Morogoro. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemkumbusha Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza ahadi yake ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwa tangu alipotangaza imepita takribani miezi miwili.

Mbowe ameeleza hayo leo Jumatano Juni 9, 2021 katika mkutano wa  baraza la maridhiano la Chadema Mkoa wa Morogoro.

Aprili 22, 2021 Rais Samia alilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo pamoja na mambo mengine alisema anakusudia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini, ili kuweka mwelekeo wa kuendesha shughuli za siasa zenye tija na masilahi kwa Taifa.

Mbowe amesema Rais Samia kukutana na Chadema pamoja na vyama vingine vya upinzani kutasaidia kupoza machungu na majeraha yaliyotokea kwa vyama hivyo kwa muda mrefu na kutaimarisha ushirikiano baina ya Serikali na vyama vya siasa.

Mbowe alitaja baadhi ya mambo ambayo Chadema imepanga kueleza endapo watakutana na Rais Samia kuwa ni  machungu wanayopitia baadhi ya wananchi na viongozi wa siasa yaliyosababishwa na watendaji wachache ndani ya Serikali bila kuchukuliwa hatua.

"Tunamuomba Rais kama ambavyo aliazimia kukutana nasi viongozi wa vyama vya siasa basi ni vema angetueleza azma hiyo kama bado anayo ili nasi tukutane naye kuzungumza kwa maslahi mapana ya Taifa.” Amesema Mbowe.

Advertisement

Amesema watamshauri aunde kamati ya upatanishi itakayofanya kazi ya kusikiliza vilio vya walioteswa na kunyanyasika kisiasa na baadaye ifanye usuluhisho ili Taifa lisonge mbele.

Imeandikwa na Hamida Shariff, Mwananchi

[email protected]
Advertisement