Mbowe amtahadharisha Rais wanaojiita ‘chawa wake’

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Mwenyekiti Chadema, Freeman Mbowe amesema amechagua kusema ukweli na kukataa dhambi ya unafiki, huku akisisitiza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa makini na watu wanaojiita chawa wake.

Hayo ameyasema leo wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema yaliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
 Mbowe amesema wamelipa gharama kubwa kwa misingi na misimamo hiyo. Amesema wao Chadema wanaamini katika ukweli, uwazi, kutokuwa wanafiki ndiyo njia bora ya kusaidia kusonga mbele.

“Hatutokuwa wanafiki ili uweze kuwa kiongozi bora, tutasema ukweli ndiyo njia bora ya kuisaidia serikali iweze kutekeleza wajibu wake,” amesema.

“Sisi kama chama kikuu cha upinzani tutaishi maisha hayo bila woga wowote, bila unafiki, bila kujikomba bila uchawa tutanyoosha na tutasema kama inavyostahiki,” amesema.

“Kwa sababu tunaamini hiyo ndiyo njia sahihi ya kuwatengenezea watoto na watoto wa watoto wetu Taifa bora siku zijazo kwa kizazi kijacho. Hofu hizi lazima tuzimalize kwa vitendi, ukiwa mkuu wa nchi ukawa mkatili, mfumo mzima wa utawala wako unakuwa katili, amesema Mbowe.

“Ni matumaini yangu, Mheshimiwa Rais, azma yako ya kuliweka Taifa pamoja itarithiwa na viongozi waliopo chini yako, waliopo katika serikali yako, waliopo katika taasisi mbalimbali za utoaji haki katika Bunge, Mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama na watu wote wanaoshika katika utawala na uongozi wa watu,” amesema.

Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema nchi ni ya wananchi, lazima wakati wote vyama vikuu visikilize wananchi na kwenda pamoja kutekeleza matakwa ya Watanzania
“Watanzania wanalilia mambo mawili, hali ngumu ya maisha na katiba mpya na tume huru ya uchaguzi,” amesema.

“Mambo haya kwa safari mliyoianza kuanzia Mwenyekiti Mbowe (Freeman) alipotoka gerezani ya kuliunganisha Taifa katika haki na safari ya mwaka mzima mliyoenda nayo kwa njia mbalimbali. Naamini safari hii ikiendelea mbele kwa pamoja kama Watanzania hakika tutafika katika nchi tunayoitafuta,” amesema.