Mbowe amwandikia barua Rais Samia akitaka mwanzo mpya

Mbowe amwandikia barua Rais Samia akitaka mwanzo mpya

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amesema amemwandikia barua Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuomba kukutana naye pasipo kutumia mwamvuli wa kiasiasa na kwamba lengo ni kutafuta ufumbuzi utakaolitoa taifa kwenye mkwamo na kurejesha furaha, haki na ustawi wa watu.

Dar es Salaam. Katika kutafuta ufumbuzi utakaoliletea taifa furaha, haki na ustawi, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amesema amemwandikia barua Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.


Mbowe ameyasema hayo leo Jumapili Aprili 11, 2021 wakati akilihutubia Taifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.


“Nimemwandikia barua Mama Samia. Pamoja na mambo mengine mengi, nimemweleza kuwa maneno yake haya yamegusa mioyo ya wengi wenye hofu ya Mungu ikiwemo sisi Chadema. Ijapokuwa bado mioyo yetu inavuja damu, tumepokea ahadi yake hii kwa tahadhari kubwa.


“Tumemwomba rasmi kukutana naye tuweze kumweleza ni namna gani mioyo yetu inavuja damu macho yanabubujikwa machozi,  hatukusudii kumzingua na hatutarajii kuzinguliwa, hatupo katika mtizamo wa kisiasa bali tunautafuta ufumbuzi utakaotutoa kwenye mkwamo huu na utakaorejesha furaha, haki na ustawi kwa watu wetu wote,” amesema Mbowe.


Amesema wanategemea kumweleza na kumkabidhi mapendekezo yeo kadhaa ya kina ya namna gani bora ya kuuanza upya katika adhma ya kujenga utengamano wa nchi na wanaamini atatambua nafasi ya vyama vya upinzani.
Aidha katika hatua nyingine Mbowe alipongeza uamuzi wa Rais wa kufikiria upya namna ya kupambana nau gonjwa tandavu wa Corona.

Mbowe amuandikia barua Rais Samia


“Tunampongeza kwa kuunda tume kufuatilia suala hili ili tuwe na msimamo kama nchi. Tunaomba Mheshimiwa Rais afikirie namna ya kuchanganya wataalamu nchi mbalimbali wenye uzoefu katika kukabiliana na suala hili,” amesema Mbowe.