Mbowe apata chanjo ya corona

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe aweka wazi kuwa amepata chanjo ya kukabiliana na corona wakati alipokuwa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi minne.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametamka hadharani kuwa amepata chanjo ya kukabiliana ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona wakati alipokuwa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi minne tangu Desemba mwaka jana.

Mbowe ameeleza hayo leo Jumapili Aprili 11, 2021 wakati akihutubia wananchi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo yaliyojitokeza katika utawala wa awamu ya tano iliyoongozwa na hayati John Magufuli aliyefariki dunia, Machi 17, mwaka huu.

Ameeleza hayo katika hotuba yake wakati akizungumza hatua zilizochukuliwa na rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan kuhusu mapambano ya Covid-19 akimtaka kuharakisha suala hilo. 
 
Hivi karibuni akizungumza katika hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa taasisi za Serikali, Rais Samia alisema ataunda kamati ya wataalamu itakayofanya tathimini ya maambukizi ya ugonjwa wa corona kisha kuishauri Serikali njia ya kufuata.