Mbowe atema nyongo

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitema nyongo baada ya kuwa kimya kwa zaidi ya miezi minne, akisema alikuwa nchi za nje kwa shughuli za biashara.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe juzi alitema nyongo baada ya kuwa kimya kwa zaidi ya miezi minne, akisema alikuwa nchi za nje kwa shughuli za biashara.

Mwenyekiti huyo, alieleza hayo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wake uliokuwa ukirushwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kabla ya kueleza kinaga ubaga yanayomsibu akisema miaka mitano iliyopita imetoa somo kwa Watanzania na jumuiya za kimataifa.

Kwenye mkutano huo, Mbowe alieleza kusikitika kutohudhuria msiba wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 katika hospitali ya Mzena Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na kuzikwa kijijini kwake Chato lakini akasema Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alimwakilisha ipasavyo.


Mazuri ya JPM

Katika hotuba yake, Mbowe alianza kwa kueleza masuala mbalimbali yaliyokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa na Watanzania kwa ujumla yaliyofanywa na Hayati Magufuli, akisema kiongozi huyo atakumbukwa kwa mengi mazuri japo na mabaya hayakosekani.

“Sifa za kipekee za Hayati Magufuli moja ni uthubutu wa kufanya maamuzi magumu. Alikuwa na uwezo wa kufanya uamuzi mgumu ambapo busara za kawaida za binadamu zisingeweza kufanya.

“Alikuwa mchapakazi na alisisitiza watu kufanya kazi, aliishi kwenye filosofia ambayo pia Chadema tunaamini ya asiyefanya kazi na asile. Hapa sijadili maisha yake binafsi, namjadili aliyekuwa Rais wa nchi mwenye dhamana ya kulinda uhuru, haki na maendeleo ya wananchi,” alisema Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Jimbo la Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.

Kuhusu udhaifu wa Hayati Magufuli Mbowe alisema; “Najua maneno yangu leo (jana) hayatafurahisha baadhi ya watu, lakini wengi watatafakari kama mimi nilivyotafakari pamoja na chama changu. Nasema bila woga kama vile ambavyo yeye (JPM) alivyokuwa hai.

“Nililipa kwa gharama kubwa kutokana na msimamo wangu huo,” alisema aliyefichua kuwa alikwenda nje ya nchi kutokana na mazingira ya ufanyaji biashara nchini kuwa magumu wake.

Alisema kuwa aliamua kwenda nje ya nchi ingawa si kama mkimbizi wa kisiasa bali kusaka fursa katika mataifa ya Afrika Kusini, Dubai na Marekani.


Adai akaunti zake zilifungwa

Mbowe alidai kuwa juzi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilimuandikia barua ikimtaarifu kuwa akaunti zake zimefunguliwa na wameondoa zuio. Hata hivyo, alisema hatua hiyo huenda imetokana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Hivi karibuni Rais Samia alionyesha kukerwa na matumizi ya mabavu ya baadhi ya watendaji na taasisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali hasa ukusanyaji wa kodi. Pia, alieleza kuwa kuna wafanyabiashara wamekuwa wakifungiwa akaunti za benki na wengine kuchukuliwa fedha jambo ambalo amelikemea hadharani.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alipoulizwa kuhusu madai hayo ya Mbowe alisema, masuala ya kodi ni kati ya mlipakodi na mamlaka hiyo. “Sipendi kuzungumzia kwenye hilo kwa sababu mlipakodi anawsiliana moja kwa moja na sisi. Mlipakodi kama ana concern (jambo) anayo haki ya kuwasilisha lalamiko lake katika ngazi mbalimbali za mamlaka au katika vyombo vya usuluhishi wa migogoro ya kodi,” alisema Kayombo.


Rais Samia na Covid-19

Mbowe alimuomba Rais Samia kulikimbiza suala kupambana na Covid-19 kutokana na kuonyesha nia ya kukabiliana changamoto hiyo huku akibainisha kuwa yeye ameshapata chanjo alikokuwa nje ya nchi.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa taasisi za Serikali, Rais Samia alisema ataunda kamati ya wataalamu itakayofanya tathmini kisha kuishauri Serikali njia sahihi za kufuata kwa kuwa, Tanzania haiko kisiwani na ni lazima iendane na kasi ya dunia tena isiwe peke yake.


Amuandikia barua Rais Samia

Mbowe alisema Chadema kimemuandikia barua Rais Samia ikimuomba kuonana naye ili kumueleza masuala mbalimbali yaliyojitokeza ndani ya miaka mitano ikiwa ni harakati za kurejesha umoja.

“Tunategemea kumueleza na kumpa mapendekezo ya namna bora ya kuanza ukurasa mpya kwenye nyanja za uchumi, siasa na jamii katika zama za utengamano. Hatukusudii kumzingua, lakini nasi hatutegemei kuzinguliwa,” alisema.


Kauli za Rais Samia

Alisema kauli na matendo ya Rais Samia vinaashiria ni kiongozi mwenye nia njema ingawa bado wanahitaji muda kujua ukweli wake.

Machi 19, mwaka huu wakati akiapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita, Samia alisema: “Huu sio wakati wa kutazamana kwa mashaka bali ni wakati wa kutizama mbele kwa matumaini ya kujiamini. Si wakati wa kutizama yaliyopita, si wakati wa kuonyesha vidole bali wakati wa kushikana mikono,” alimaliza kunukuu Mbowe.


Katiba Mpya

Kuhusu Katiba Mpya, Mbowe alieleza hawatasubiri Rais Samia kuruhusu mchakato huo huku akisema suala hilo halihitaji utashi binafsi.

Alisema Katiba Mpya ndiyo msingi na roho ya Taifa na kwamba, halipaswi kuwa mjadala kwani kipindi hicho kilishapita na sasa ni utelelezaji.

Hata hivyo, wakati akiwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri Ikulu ya Chamwino, Rais Samia alisema suala la Katiba mpya litasubiri kwanza wakati huu akiendelea kusuka Serikali yake kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.


Kujaza makada serikalini

Mbowe alidai kuwa Serikali ya awamu ya tano ilijaza makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Serikali na kwamba, haikuwa ikiwaamini wa umma ambao hawakufungamana na chama chochote cha siasa.

Hata hivyo, Katibu wa Siasa, Itikadi na Mambo ya Nje wa CCM, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga alisema Hayati Magufuli alikuwa hateui wakurugenzi na watendaji wengine wa Serikali kwa sababu walikuwa makada bali kutokana na sifa walizokuwa nazo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Faraja Kristomus alisema mkutano wa Mbowe na Rais Samia utakuwa na matokeo makubwa kwa sababu unalenga kuleta maridhiano baina ya Serikali na vyama vya siasa nchini.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, baadhi ya viongozi waliifanya CCM kuwa chama cha daraja la juu na vyama vya upinzani vikionekana kuwa daraja la chini.

Alisema wanachama wa upinzani wakiwemo wabunge na madiwani walikuwa wanavihama vyama vyao na kujiunga na CCM kwa ajili ya kutafuta fursa, ambapo baadhi wamefanikiwa.