Mbowe awataka vijana kuwa chachu ya mabadiliko

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka Vijana kuchukua hatua na kukubali mabadiliko ili kizazi kijacho kiwe na elimu ya kuweza kushindana na mataifa mengine yaliyoendelea kimaendeleo na kielimu.

  

Shinyanga. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka Vijana kuchukua hatua na kukubali mabadiliko ili kizazi kijacho kiwe na elimu ya kuweza kushindana na mataifa mengine yaliyoendelea kimaendeleo na kielimu.

Hayo ameyasema leo Agosti 12 kwenye kongamano la Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha) lililofanyika kitaifa mkoani hapa, akiwataka vijana kujitathimini na kuchukua hatua ya mabadiliko kwa ajili ya kizazi kijacho.

Mbowe amesema vijana wengi hawana ajira kwa sababu ya kukosa elimu sitahiki, huku wazazi wao wakiwa na kipato cha dola 1 kwa siku isiyowawezesha kujikimu kimaisha.

"Kila mtoto anazaliwa na akili lakini anatakiwa kuwa na elimu bora, tuna watoto milioni 1.4 wasiokuwa na ajira tumeruhusuje?

“Maana kila mwaka wanaingizwa mitaani na mwenye wajibu wa kuhakikisha watoto hawa wanapata elimu ni serikali iliyopo madarakani inapasa kuwajibika," amesema Mbowe.

Amewataka vijana kutumia umri wao vizuri kwa kusaidia watoto na wazee.

“Acheni kuwa wakali piganieni maendeleo kupigania kuwa na uchumi bora ili kuondokana na umasikini uliopo.

"Vijana wangu jitengenezeeni kesho yenu msiwe watu wa kulalamika kila wakati, na wale ambao hamkuipata elimu bora msikate tamaa mnapaswa kupambana na kutambua wajibu wenu," amesema Mbowe.

Awali akizungumza katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesisitiza umuhimu waa kupatikana kwa katiba mpya, akisema ni hitaji muhimu la Watanzania.

"Ili Tanzania tupate uchaguzi huru wa haki ni vizuri tusimamie katiba mpya ili tuweze kupata bunge huru, hivyo viongozi wote wa Chadema tunatakiwa tuongeze nguvu ili tuwe na tume huru na katiba mpya na tuongeze zoezi la usajili wa chama," amesema Mnyika.

Aidha Mnyika amesema Vijana wote ambao wanatarajia kuwa viongozi ndani ya Chadema waanze kuwekeza ndani ya chama kwa sababu kauli mbiu yetu inasema vijana ni Taifa la leo.

Pia Mnyika amewataka vijana wa kike na wakiume wajitokeze kugombea kwenye serikali za mtaa ili waweze kutetea Taifa lao na kuwa mstari wabele katika kuongoza.


Naye Naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu amesema Watanzania wanataka katiba mpya ikazalishe mambo mbalimbali ikiwemo serikali tatu.

"Baadhi ya watu wanasema ni gharama kuwa na serikali tatu, lakini hakuna gharama zinazoongezeka kwa sababu zanzibar kuna makamu wa rais na huku kuna makamu wa Rais Zanzibar kuna Jaji mkuu na huku kuna jaji mkuu  hivyo hakuna kitakachoongezeka," amesema Mwalimu.