Mbowe na Lissu wawasubiri Halima Mdee na wenzake

Friday November 27 2020
kamatipic
By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza kwa ajili ya kuwajadili wanachama 19 walioapishwa Novemba 24, 2020 kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama hicho.

Kikao hicho kinachofanyika leo Ijumaa Novemba 27, 2020 jijini Dar es Salaam kinaongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wengine waliohudhuria ni makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohammed; katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika naibu wake Zanzibar, Salum Mwalimu huku makamu mwenyekiti bara, Tundu Lissu akishiriki kwa njia ya mtandao.

Hata hivyo hadi saa 7:00 mchana walengwa wanaotakiwa kuhojiwa ambao ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso,  Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed,  Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest,  Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza walikuwa hawajafika.

Wajumbe wengine wa kikao hciho waliofika ni John Heche, Mchungaji Peter Msigwa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, Boniface Jacob, Suzan Kiwanga, John Mrema, Julius Mwita, Rodrick Rutembeka, Patrick Ole Sosopi, Hashim Juma na  John Pambalu.

Juzi, Mnyika alitangaza kuwa kamati kuu ya chama hicho itakutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwahoji wabunge hao wa viti maalumu, pia, aliwataka wabunge hao kuhudhuria kikao hicho.

Advertisement

Mnyika alisisitiza kwamba Kamati Kuu ya Chadema ambayo ndiyo ina mamlaka kikatiba ya kupendekeza wabunge wa viti maalumu, haijakutana kufanya hivyo wala kutuma majina kwa Tume kwa Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa uteuzi.

Tangu kuapishwa kwao kumekuwa na sintofahamu kuhusu suala hilo, hasa baada ya viongozi wa Chadema kuweka msimamo wa kutoteua viti maalumu kuto-kana na kutoyatambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28.

Baada ya uchaguzi, Chadema pekee ndicho chama cha upinzani kilichokidhi vigezo vya kupata wabunge wa viti maalumu baada ya kufikia asilimia tano ya jumla ya kura za wabunge.

Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kushangazwa na hatua ya kuapishwa kwa makada wake kuwa wabunge wa viti maalumu bila baraka zake.

Advertisement