Mbunge acharuka Serikali kutwaa eneo bila kufuata utaratibu

Muktasari:

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Dk Oscar Ishengoma amekataa kuunga mkono hoja bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi mwaka 2022/2023 hadi hapo Serikali itakapotoa ufafanuzi kuhusu vitongoji 19 wilayani Muleba mkoani Kagera vilivyotwaliwa bila kufuata utaratibu.

Dodoma. Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Dk Oscar Ishengoma amekataa kuunga mkono hoja bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi mwaka 2022/2023 hadi hapo Serikali itakapotoa ufafanuzi kuhusu vitongoji 19 wilayani Muleba mkoani Kagera vilivyotwaliwa bila kufuata utaratibu.

 Dk Ishengoma ameyasema hayo leo Jumatano Mei 25 wakati akichangia katika mjadala wa makadirio ya mapato ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema ardhi hiyo ilichukuliwa na Ranchi za Taifa (Narco) ambao wamevamia eneo hilo lililopo Mwisa na Lutoro bila kufuata utaratibu wa kisheria wa kutoa notice ya kuwataka kuhama.

“Wakazi hawa wako katika kilio. Kazi ya mama ni kupangusa wa machozi. Tunamuomba awapanguse machozi wakazi wa vitongoji 19 ambao maeneo yametwaliwa bila notice ya Serikali tunashindwa kuelewa nchi inapelekwa wapi,”amesema.

Amesema ardhi hiyo ilichukuliwa kinyume cha utaratibu hakuna notice na hivyo kumtaka Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki kueleza Bunge wameipataje na notice ni namba ngapi.

“Wananchi wananyanyaswa, wanahamishwa hakuna hata mtu anafuata hata sheria ya kuhamisha makaburi, mnalishia katika makaburi ya wazazi wetu, hatuwezi kukubali kama hakuna notice tuwatangazie waendelee kuishi hadi utaratibu utakapofuatwa,”amesema.