Mbunge afananisha urasimu na mafuta ya upako

Mbunge afananisha urasimu na mafuta ya upako

Muktasari:

Mbunge wa Iringa mjini Jeska Msambatavangu ameliambia Bunge kuwa  licha ya mpango mzuri wa Serikali lakini unaweza kukwama kutokana na urasimu mkubwa uliopo Tanzania.

Dodoma. Mbunge wa Iringa mjini Jeska Msambatavangu ameliambia Bunge kuwa  licha ya mpango mzuri wa Serikali lakini unaweza kukwama kutokana na urasimu mkubwa uliopo Tanzania.

Msambatavangu ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Aprili 9,2021 wakati akichangia bungeni hoja ya mpango wa Serikali ambapo amesema kuna urasimu na ukiritimba mkubwa katika idara na Taasisi za Serikali aliouita ni utelezi sawa na mafuta ya upako.

"Mpango ni mzuri,lakini utakwamishwa na urasimu mkubwa ambao watendaji wetu wanao kwani inakuwa vigumu watu kuwekeza hata kufanya mambo yao kutokana na mzunguko ambao unafika mwisho kwa watu kukata tamaa," amesema Msambatavangu.

Mbunge huyo ameeleza ilivyo vigumu kupata vibali, hati za kusafiria, visa na nembo za wakala wa viwango ukilinganisha na mataifa mengine.

Amesema utelezi mwingine upo kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wanashindwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara badala yake wanasubiri wakosee ili wawapeleke mahakamani.