Mbunge alilia fidia za wananchi Makambako

Mbunge wa Makambako, Deo Sanga

What you need to know:

Mbunge wa Makambako, Deo Sanga ameoamba Wananchi waliopisha miradi ya maendeleo wamaliziwe fidia ili wafanye maendeleo binafsi.

Dar es Salaam. Mbunge wa Makambako, Deo Sanga ameomba wananchi waliopisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo wamaliziwe fidia zao ili waweze kufanya maendeleo.

 Miongoni mwa wanaodai fidia ni wale waliopisha mradi wa ujenzi wa umeme wa upepo, waliopisha ujenzi wa kituo cha huduma za pamoja (One stop Center) na waliopisha ujenzi wa kituo cha polisi.

Ameyasema hayo leo wakati akitoa salamu za wananchi wake kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliposimama katika eneo la Makambako akiwa njiani kuelekea mkoani Iringa akitokea Njombe.

Amesema kituo cha polisi kwa sasa kinafanya kazi vizuri lakini wapo watu waliochukuliwa maeneo yao na wanahitaji kulipwa fidia.

“Leo Waziri wa Mambo ya Ndani yuko hapa, Mama muagize awalipe wananchi hawa, kwani nyumba zimebomoka na hawawezi kufanya kitu chochote, utakuwa umetusaidia sana,” amesema Sanga.

Kuhusu waliopisha ujenzi wa One stop center katika eneo la Idofi, amesema Sh870 milioni zimeshalipwa lakini kuna fedha ambayo haijamaliziwa hivyo aliomba mchakato wake ukamilike.

Katika kushughulikia hilo, amesema amekuwa akiwasaliana kwa karibu na Waziri Makame Mbarawa wa ujenzi na Uchukuzi.

“Pia kuna Wananachi waliopisha mradi wa umeme wa upepo, walizuiliwa wasifanye chochote sasa wanasubiri fidia, hawawezi kufanya chochote, niliwasiliana na Waziri Januari Makamba (Nishati) nikaambiwa mwishoni mwa mwezi huu tunaweza kupata majibu tunaomba na hili lichukuliwe,” amesema.

Akijibu suala la fidia kwa waliopisha ujenzi wa kituo cha polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema ulipaji wa fidia ulikumbwa na changamoto baada ya kaya 14 zilizofanyiwa tathmini kugoma.

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa tathmini awali ilikuwa ni kuwalipa Sh89 milioni lakini waligoma kwa sababu tathmini ilihusisha shughuli za kimaendeleo walizokuwa wamefanya haukuhusisha ardhi.

“Tathmini ile irudiwa na kufikia Sh209 milioni, niwahakikishie kuwa fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu, msiwe na wasiwasi na fedha hizi zitalipwa kwa wakati wowote kuanzia sasa,” amesema Masauni.

Waziri wa Ujenzi, Makame Mbarawa amesema tayari takribani Sh870 milioni zimelipwa kwa watu ambao walichukuliwa maeneo yao huku Sh2.9 bilioni ikiwa mbioni kumaliziwa.

“Hakuna mtu atakayepoteza haki yake, kama haki yako unatakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria utaipata, nawaomba wale ambao hawajilipwa fidia mjue haki yenu ipo na hamtadhurumiwa,” amesema Mbarawa.

Kuhusu waliopisha ujenzi wa Onestop Center, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema wameshapokea suala hilo kupitia barua ya Waziri wa ujenzi na Uchukuzi.

“Tunafanyia kazi na pindi taratibu za malipo zitakapokamilika tutaweza kutekeleza suala hili, hivyo wananchi wa Njombe endeleeni kuwa na subira tunakamilisha taratibu za malipo,” amesema Dk Mwigulu.