Mbunge anayedaiwa kuua atoroka

Mbunge wa jimbo la Kamilikwa, Didmus Barassa

Muktasari:

  • Mbunge wa jimbo la Kamilikwa, Didmus Barassa katika Kaunti ya Bungoma, anayedaiwa kumuua kwa kumpiga risasi Brian Olunga ambaye ni msaidizi wa mgombea wa upinzani Brian Khaemba wakiwa katika kituo cha kupigia kura, anadaiwa kutorokea nchini Uganda kukwepa mkono wa sheria.

Nairobi. Mbunge wa jimbo la Kamilikwa, Didmus Barassa katika Kaunti ya Bungoma, anayedaiwa kumuua kwa kumpiga risasi Brian Olunga ambaye ni msaidizi wa mgombea wa upinzani Brian Khaemba wakiwa katika kituo cha kupigia kura, anadaiwa kutorokea nchini Uganda kukwepa mkono wa sheria.

Tukio hilo limetokea juzi jioni, kwenye kituo cha kupiga kura cha shule ya msingi Chebukhwabi ambapo Khaemba na wasaidizi wake walienda kwa ajili ya kusimamia uhesabuji wa kura.

Mashahidi wa tukio hilo walisema kuwa mgombea huyo wa ubunge wa chama cha DAP-K alipokuwa anatoka kituoni hapo na wasaidizi wake walifuatwa na Barassa akiwa na watu wanne na kuwaamuru wasimruhusu kuondoka, lakini dereva wa Khaemba alikaidi na kuwasha gari.

Kitendo hicho kilimfanya Barasa atoe bastola na kumlenga msaidizi mmoja wa Khaemba aliyetambulika kwa jina la Brian Olunga na kumpiga risasi kwenye paji la uso na kusababisha mauti yake wakati akiwa mbioni kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo cha polisi cha Kimili, Kamishna wa Kaunti hiyo, Samuel Kimiti amesema wanaendelea kumtafuta mbunge huyo.

“Tunamtaka ajisalimishe kituo chochote cha polisi popote alipo. Mwananchi yeyote akimuona atoe taarifa polisi,” amesema.
Kimiti aliongozana na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, ambaye pia amelaani tukio hilo na kuwataka polisi wamkamate mbunge huyo haraka.

Polisi walionyesha hofu kwamba mbunge huyo huenda amekimbilia nchini Uganda.