Mbunge apendekeza wabunge wafunge fedha za Kilimo zitolewe zote

Muktasari:

Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole ametoa pendekezo kwa wabunge wenzake kufunga kwa maombi ili fedha zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2022/23 zitolewe zote.

Dodoma. Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole ametoa pendekezo kwa wabunge wenzake kufunga kwa maombi ili fedha zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2022/23 zitolewe zote.

Mwenisongole ametoa kauli hiyo bungeni leo Mei Jumatano 18, 2022 wakati akichangia hotuba ya Makadilio ya Mapato na matumizi kwa Wizara hiyo kwa mwaka 2022/23.

Katika kujenga hoja yake, mbunge huyo amesema tangu Tanzania ipate Uhuru, bajeti ya mwaka huu pekee ndiyo inayoakisi maisha ya wakulima kutokana na kutenga fedha nyingi kwenda kwa wakulima walengwa.

Hata hivyo amesema hofu yake ni fedha kutokutolewa kwa wakati na kiwango chote kama ambavyo imekuwa ikitokea mara nyingi kwenye bajeti za Serikali ikiwemo bajeti ya kilimo ya 2021/22.

“Ili tupate fedha hizo, napendekeza wabunge tufunge kwa maombi ili kuifanya Serikali ikumbuke kutoa fedha zote katika Wizara ya Kilimo ili kusudi ziwasaidie wakulima wetu ambao kwa miaka mingi hawajawahi kuona bajeti kama hii,” amesema Mwenisongole.

Pia, amependekeza kutungwa kwa sheria ya Kilimo ili kupambana na watu ambao wanauza mbolea na mbegu feki ambazo huuzwa mitaani na akasema kama Serikali haitapeleka bungeni Muswada wa sheria hiyo, yeye (Mwenisongole) atapelekea hoja binafsi.

Amezungumzia uimarishaji wa kilimo kwa kuwasaidia wakulima ili Serikali inufaike na kuomba Serikali iongeze nguvu zaidi kwenye Kilimo ambacho kinaajiri kundi kubwa la wananchi.