Mbunge ashauri TTCL ijiondoe kwenye ushindani

Friday May 20 2022
Ttcl pc
By Kelvin Matandiko

Dar es Salaam.  Mbunge wa Jimbo la Lupa, Chief Masache Njelu Kasaka ameshauri Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) iondolewe kwenye ushindani wa huduma za mawasiliano nchini.

Amesema kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), TTCL inashika nafasi ya sita kati ya Kampuni saba zinazotoa huduma za mawasiliano nchini, ikichangia asilimia 1.7 tu ya soko. 

Ameshauri kutokana na mazingira hayo magumu ya ushindani, serikali ijiondoe kwenye ushindani huo na kufanya mageuzi ya kisheria kuwezesha TTCL kusimamia miundombinu ya minara yote nchini.

Kasaka ametoa kauli hiyo leo Mei 20, 2022 wakati akichangia mjadala katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia kikao cha 27 cha Mkutano wa saba wa Bunge linaloendelea mjini Dodoma.

“Kutokana na mazingira magumu ya kiushindani, tuwe na sheria inayoweza kuwabeba ili waweze kufanya kazi yao vizuri. Ili kuweza kusaidia TTCL tubadili sheria ili wabakie kuwa wajenzi wa miundombinu pekee, wasiingie kama washindani kwa sababu wameonyesha hawawezi,” amesema.

“Wanapewa minara yote na mingine waendelea kuijenga, baada ya hapo hawa operators (kampuni za simu) wapangishwe na TTCL, mnara mmoja upangishwe kwa kampuni tatu hadi nne, itasaidia minara kuwa michache na huduma zitapatikana vizuri na kwa wakati.”

Advertisement

Akijenga hoja hiyo amesema TTCL imekuwa ikipata idadi kubwa ya minara inayojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) lakini wamekuwa wakijiendesha kwa hali ya kusuasua hatua inayotishia kufikia malengo ya serikali kufikisha huduma kwa wananchi wengi.

Advertisement