Mbunge ataka ruzuku, posho kwa wanafunzi zipandishwe

Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  •  Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega ameishauri Serikali kuongeza kiwango cha fedha katika posho kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili wamudu gharama za maisha.


Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega ameishauri Serikali kuongeza kiwango cha fedha katika posho kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili wamudu gharama za maisha.

Grace ameyasema hayo leo Alhamis Juni 16, 2022 wakati akichangia Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.

Amesema wanafunzi wa vyuo vikuu wamekuwa wakipewa posho ya Sh8500 wakati dola moja ya Marekani ilikuwa ni sawa na Sh1600 hadi leo ambapo dola moja ni sawa na Sh2400 wanapata kiasi hicho hicho.

“Hadi leo wanapata kiasi hicho hicho cha fedha hapana tuwaboreshee. Lakini na mishahara imepanda tuangalie hawa vijana tuweze kuwaboreshea,”amesema.

Aidha, ametaka fedha za ruzuku ziongezwe kwa wanafunzi wa shule za msingi ambayo ni Sh10,000 angalau ifike Sh25,000.

Pia ameshauri kuongezwa kwa ruzuku kwa wanafunzi wa shule za sekondari angalau ifikie Sh50,000 ili waweze kupatiwa huduma bora za kielimu wanapokuwepo shuleni.