Mbunge ataka wanaotoa huduma zisizoridhisha kwa wajawazito kushughulikiwa

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel

Muktasari:

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amewataka wabunge kutengeneza ushahidi kwa watumishi wa sekta ya afya wanaotoa huduma zisizo bora kwa wajawazito ili washughulikiwe.

Dodoma. Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amewataka wabunge kutengeneza ushahidi kwa watumishi wa sekta ya afya wanaotoa huduma zisizo bora kwa wajawazito ili washughulikiwe.

Dk Mollel ameyasema hayo leo Jumatano Mei 25, 2022 wakati akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Agnes Hokororo.

Agnes alitaka kujua ni sheria ipi inayosimamia wajawazito wanaopata huduma isiyoridhisha ama zisizo bora.

Pia ametaka kufahamu kuwa kama ipo sheria inatoa malipo ya fidia kwa wajawazito wanapopata huduma isiyoridhisha au zisizo bora zinazosababisha athari za kiafya na hata kifo.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema zipo kanuni ambazo zinataka watoto chini ya miaka mitano na wajawazito wapatiwe huduma bure.

Amesema suala la kujibiwa vibaya ama kwa fedheha zipo sheria za kiutumishi zinaonyesha jinsi ya kushughulikia changamoto hiyo.

“Anapopatikana mtu amejibu vibaya amejibu vibaya wakati anapitishwa kwanza kwenye sheria za maadili ya kitaaluma lakini anaachiwa sheria za kimaadili zifuate mkondo huo,”amesema.

Amemtaka mbunge huyo kuendelea kutengeneza ushahidi wa kutosha ili kuwapata watu wa namna hiyo kushughulikiwa kufuata sheria.

Katika swali lake la msingi mbunge huyo alihoji kama kuna Sheria ya Huduma ya Afya inayosimamia utoaji na upatikanaji wa huduma za Afya.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema Wizara ya Afya inasimamia Sheria zipatazo 30 zinazolenga kusimamia ubora na utoaji wa huduma, maadili ya kitaaluma, kiutumishi na upatikanaji wa huduma za afya nchini.