Mbunge CCM akataa majibu ya Serikali bungeni

  • Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga akiuliza swali katika kikao cha tisa cha mkutano wa tatu wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Mbogwe (CCM),  Nicodemus Maganga ameyakataa majibu ya Serikali bungeni kuwa katika jimbo hilo wananchi wanapata maji na kuhoji vilipo visima 26 vya maji.

Dodoma. Mbunge wa Mbogwe (CCM),  Nicodemus Maganga ameyakataa majibu ya Serikali bungeni kuwa katika jimbo hilo wananchi wanapata maji na kuhoji vilipo visima 26 vya maji.

Akizungumza bungeni leo Jumatano Aprili 14, 2021 mbunge huyo amesema hakuna visima vya maji katika jimbo lake na wananchi wanaendelea kuteseka kwa kukosa maji wakati wote.

Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, naibu waziri wa maji, Maryprisca Mahundi amesema katika jitihada za kutatua tatizo la maji, Serikali ilichimba visima virefu jimboni humo na vinatumika hadi sasa.



"Sijaridhishwa na majibu ya Serikali hivyo visima vimechimbwa wapi? Mimi ni mbunge wa Mbogwe na ninaishi huko lakini sijawahi kuona hayo maji naomba kujua visima viko wapi," amehoji Maganga.

Mbunge huyo amesema majibu ya naibu waziri ni ya kwenye makaratasi aliyoandikiwa kwa kudanganywa na kumuomba aende kwenye jimbo hilo akajionee mwenyewe ombi ambalo lilikubaliwa na naibu waziri huyo.

Maryprisca  ameahidi kwenda Mbogwe kwa ajili ya kuona uwezekano wa kutumia maji ya Ziwa Victoria ili kumaliza tatizo la maji katika jimbo hilo na maeneo jirani.