Mbunge CCM akosoa ujenzi reli ya kisasa

Thursday April 08 2021
By Habel Chidawali

Dodoma. Mbunge wa Handeni (CCM), Reuben Kwagila amelieleza Bunge leo Alhamisi Aprili 8, 2021 kuwa bila kubadili mtazamo wa ujenzi  wa reli ya kisasa (SGR), itajengwa kwa miaka 81.

Amesema aina ya ujenzi inayofanyika Tanzania ni wa kuwapa presha viongozi  na kushindwa kuwahudumia wananchi katika mambo ya msingi.

Kwagila ametoa kauli hiyo bungeni wakati akichangia mpango wa Serikali wa miaka mitano uliwasilishwa mapema leo na Waziri wa Fedha na Mipango,  Dk Mwigulu Nchenba.

Mbunge huyo amesema kilomita 4,886 zinazotakiwa kujengwa hazitafikiwa kwa kutumia fedha za ndani kwani hata nchi zilizoendelea hawajengi miradi mikubwa kwa fedha za ndani.

"Tutaendelea kuwa na presha kubwa huku wananchi nao wakikosa huduma muhimu na Taifa linaendelea kupata hasara kubwa," amesema Kwagila.

Mbunge huyo ameishauri Serikali kujenga reli hiyo kwa kutumia alichokiita kukopa kwa ajili ya kujenga miradi, akisisitiza kuwa itachukua muda mfupi kukamilisha miradi na faida itaonekana.

Advertisement

Amesema Tanzania haiwezi kukamilisha kujenga SGR kwa kutegemea mapato yake ya ndani kwa kuwa itachukua muda mrefu.


Advertisement