Mbunge CCM awataja mawaziri akizungumzia taulo za kike

Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga.

Muktasari:

  • Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amepeleka kilio cha uhaba wa taulo za kike kwa wanawake sita akiamini kuwa ni shupavu wanaweza kulibeba suala hilo kwa uzito na kuwarejeshea tabasamu baadhi ya wasichana, hasa wanafunzi.

Dodoma. Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amepeleka kilio cha uhaba wa taulo za kike kwa wanawake sita akiamini kuwa ni shupavu wanaweza kulibeba suala hilo kwa uzito na kuwarejeshea tabasamu baadhi ya wasichana, hasa wanafunzi.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma leo Jumanne Mei 4, 2021 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu mwaka 2021/22 iliyowasilishwa bungeni na Profesa Joyce Ndalichako, Sanga amesema haamini kama wanawake hao watashindwa.

"Spika tunao wanawake shupavu kabisa nianze na Rais Samia Suluhu Hassan na mawaziri Profesa Ndalichako (Elimu), Ummy Mwalimu (Tamisemi), Jenista Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu), Dk Dorothy Gwajima (Afya) na Naibu Spika Dk Tulia Akson, lazima mlibebe hili kwa nguvu zote,” amesmea

Amebainisha kuwa taulo za kike limekuwa janga kwa madai kuwa huwakosesha wanafunzi vipindi darasani, kama Serikali itaamua kutoa msukumo wa dhati wa taulo hizo kwa wanafunzi, hakutakuwa na shida.

Huku akinukuu taarifa za shirika la kimataifa la kuhudumia watoto duniani (Unicef), mbunge huyo amesema watoto wengi hupoteza vipindi kati ya siku mbili hadi tatu wakiwa katika hedhi.