Mbunge, wananchi waanza mchakato ujenzi wa shule

Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga na wananchi wa Kijiji cha Itonya Kata ya Kimala wakisomba mawe kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule mpya ya sekondari.

Muktasari:

  • Hatua ya Serikali kutenga Sh600 milioni katika bajeti ya 2024/25 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kata ya Kimala imesababisha wananchi na Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga kusafisha eneo la ujenzi.

Iringa. Baada ya kilio cha muda mrefu cha kukosekana kwa shule ya sekondari katika vijiji vya Itonya, Uluti na Mhanga vilivyopo Kata ya Kimala mkoani Iringa, Serikali imetenga Sh 600 milioni katika bajeti ya 2024/25 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Mbunge wa Kilolo (CCM), Justin Nyamoga ameongoza wananchi kusafisha eneo la eka 15 litakalojengwa shule hiyo.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kumalizika kwa kazi hiyo, Nyamoga amesema ili kupunguza gharama za ujenzi baadhi ya kazi zinapaswa kufanywa na wananchi.

 “Sio kwamba nimekuja kupiga picha, nataka wananchi waone kama kazi hizi tukizifanya wenyewe fedha zitatosha. Gharama za kununua tofali, kusafisha eneo kama tulizofanya leo zitapunguza gharama na tutafikia malengo,” amesema Nyamoga.

“Kilio cha sekondari kwenye vijiji hivi kilikuwa kikubwa na watoto walikuwa wakitembea umbali mrefu, naishukuru Serikali kupitia mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari na sisi tumeshajiandaa kupokea.”

Nyamoga amesema ujenzi wa shule hiyo mpya utakuwa na vyumba vinane vya madarasa, jengo la utawala, maabara tatu za fizikia, kemia na baiolojia.

Majengo mengine ni vyoo vya walimu na wanafunzi, jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na nyumba ya mwalimu.

Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wamesema licha ya kuwa kata yao ya Kimala ina shule,  umbali baina ya kijiji na kijiji umesababisha watoto watembee umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.

“Tulipoona mbunge anakuja tukaamini kwamba kweli fedha zimetengwa, shule hii itakuwa mkombozi mkubwa kwa watoto wetu ambao walikuwa wanatembea zaidi ya kilometa nane kwenda shuleni,” amesema Anna John, mkazi wa Kimala.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Ester Ndali amesema sio watoto wa kike peke yao waliokuwa hatarini kwa kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, hata wa kiume walikuwa wanapitia kipindi kigumu.