Mbwa kichaa ajeruhi wanafunzi watatu, mmoja afariki dunia
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Kijiji cha Wama, Japhet Tarimo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo mwanafunzi ajulikanaye kwa Jina la Denis Evod (12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano alipoteza maisha.
Rombo. Mbwa anayedhaniwa kuwa na kichaa amevamia Shule ya Msingi Wama, iliyopo Tarakea, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro na kujeruhi wanafunzi watatu huku mmoja akipoteza maisha.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Wama, Japhet Tarimo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo mwanafunzi ajulikanaye kwa Jina la Denis Evod (12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano alipoteza maisha.
Mwanafunzi huyo alifariki dunia siku ya Jumanne Februari 21, mwaka huu baada ya kung'atwa na mbwa huyo Januari 25.
Amesema baada ya tukio hilo kutokea wanafunzi hao walikimbizwa katika Kituo cha Afya Karume kupatiwa chanjo ambapo mtoto mmoja hali yake ilibadilika ghafla na kufariki dunia.
"Mwanafunzi mmoja ambaye alikuwa ameng'atwa Zaidi, baadaye hali yake ilibadilika na kuwa mbaya baada ya kupatiwa chanjo zote tatu, kwa hiyo huyu mwanafunzi baadaye alipoteza maisha,"
Akielezea tukio lilivyotokea, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Seprina Kimario amesema baada ya mtoto wake kung'atwa na mbwa shuleni walitumwa wanafunzi nyumbani kwake na mmoja wa walimu wa shule hiyo kwenda kumchukua mwanaye ili ampeleke hospitali.
"Nilifika shuleni kumchukua mwanangu japo nilikuwa sina fedha, niliomba msaada wa bodaboda aliyekuwa anapita njiani akanisaidia, nilipofika hospitali nilikaa hadi jioni mwanangu ndio akapewa chanjo," amesema.
"Alichomwa chanjo zote tatu, ambapo ilipofika siku ya tarehe 18 mwezi huu mwanangu alinambia anaumwa kichwa, kukaa kidogo akanambia sehemu ya kuanzia kiunoni kwenda chini hana nguvu nilimkimbiza Kituo cha Afya Karume akapewa dawa ya maumivu hadi kesho yake alipozidiwa na kupoteza maisha," amesema.
Amesema kwa sasa wapo kwenye kikao cha maandalizi ya mazishi na wanatarajia kuzika siku ya Jumatano Machi Mosi, mwaka huu.