Mc Pilipili asimulia jinsi ajali ilivyochukua uhai wa mama yake mzazi

Monday December 21 2020
mcpilipilipic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Msanii wa vichekesho nchini Tanzania, Emanuel Mathias maarufu MC Pilipili amesema mama yake mzazi na mama yake mdogo wamefariki  dunia katika ajali ya gari muda mfupi baada ya kutoka kanisani.

“Baada ya kupiga picha mama akiwa na mdogo wake ambaye ni mama yangu mdogo waliondoka kanisani kwenda nyumbani kuchukua nguo za kubadilisha kisha kwenda ukumbini lakini kabla hawajafika walipata ajali,” amesema msanii huyo akibainisha kuwa harusi hiyo ilikuwa ya mdogo wake na yeye ndio alikuwa msherekeshaji.

“Sekeseke lilianzia kwangu kwani nilipofika ukumbini niliona nimesahau majina ya watu wenye kadi za harusi hivyo nikachukua bodaboda kwenda nyumbani lakini wakati narudi nilianguka na kuumia kiasi nikajifuta na kurudi tena ukumbini.”

“Kabla sherehe haijaanza mama alimwambia kaka yangu kwamba anataka akachukue nguo ya kubadilisha pamoja na zawadi alizokuwa amepanga kuzitoa kwenye harusi kaka akamwambia asubiri lakini yeye akamuita mama yangu mdogo wakaondoka bila kutuaga, alifanya hivyo kwa upendo kwa sababu alitaka mdogo wangu afurahi katika harusi yake,” amesema Pilipili.

Amesema wawili hao waliondola walipofika eneo linaloitwa kituo kipya ilitokea bodaboda nyingine iliwagonga na walianguka na kufariki dunia.

“Baada ya kupigiwa simu kuhusu ajali nilisumbuka sana kwa sababu kuna wakati nilikuwa natoka nje nalia kisha narudi tena ndani na kuendelea na shughuli kwa sababu watu waliokuwa wamekuja kwenye sherehe walikuwa wanatarajia kwamba MC Pilipili anachekesha na sikutaka kuwaangusha.”

Advertisement

“Nilikuwa nimepania kumpa zawadi mama yangu katika harusi ya mdogo wangu kwa sababu kwenye harusi yangu ilishindikana, unapotaka kufanya kitu kizuri cha kumfurahisha mtu jitahidi ukifanye sasa hivi maana nilikuwa nikisema kwa muda mrefu ningemfanyia hivyo mama yangu lakini sikufanikiwa na hivi sasa siwezi tena,” amesema Pilipili.

Advertisement