Mchakato ubunge Eala washika kasi

Mchakato ubunge Eala washika kasi

Muktasari:

Mchakato wa ndani wa kuwapata wagombea watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala), umezidi kushika kasi katika vyama mbalimbali vya siasa, vikiwemo vya CCM, ACT-Wazalendo na CUF.

Dar/Dodoma. Mchakato wa ndani wa kuwapata wagombea watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala), umezidi kushika kasi katika vyama mbalimbali vya siasa, vikiwemo vya CCM, ACT-Wazalendo na CUF.

Uchaguzi wa kuwapata wabunge hao wanaotokana na CCM pamoja na vyama upinzani, unatarajiwa kufanyika katika kikao kijacho cha Bunge ambapo wabunge watapiga kura kuwapata wawakilishi hao.

Tayari vyama vya CCM, ACT-Wazalendo na CUF vimeshaanza kutoa fomu kwa wanachama wao kuwaomba kujitokeza kuchukua, ili kuipeperusha bendera ya chama husika katika uchaguzi huo.

Hadi juzi wanachama 64 wa CCM walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba kugombea kuwania nafasi hizo.

Idadi hiyo ni kubwa kulinganisha na nafasi zilizopo ambazo kila nchi inatakiwa kupeleka wabunge tisa, lakini kwa mgawanyo wa vyama, ikiwemo vya upinzani kuwa na uwakilishi bungeni. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Oganaizesheni, Maudline Castico alisema jana uchukuaji fomu unaendelea hadi Agosti 10.

Kwa mujibu wa Castico, jumla ya wanachama 16 jana walijitokeza kuchukua fomu ambapo katika ofisi kuu ya CCM Dodoma walichukua watu saba, ofisi ndogo ya CCM Lumumba Dar es Salaam walikuwa wanane na Zanzibar mmoja.

Aliwataja baadhi ya wanachama hao kuwa ni Nasikiwa Berya, Amina Mgeni, Ambwene Kajura, Nasser Nzamba, Prakseda Marmo, Maria Kangoye, Shogo Mlozi, Godfrey Shirima, Dk Paul Anthony, Henry Bulengera, James Kasurura, Alfa Munyi, Manase Michael, Ayubu Lemilya na Nicksoni Kahimba na Haji Vuai Ussi.

Naye Katibu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa ACT-Wazalendo, Mohammed Masaga alisema wanachama sita wamejitokeza kuchukua fomu, akiwemo Katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, Emmanuel Mvula, Twaha Taslima, Vincent Saguda, Mbaraka Chilumba na Samuel Sebastian.

“Mwisho wa kuchukua fomu ni Agosti 24, baada ya hapo idara ya uchaguzi itafanya uhakiki kwa wagombea waliojitokeza kama wamekidhi vigezo, kisha kuyapeleka katika kamati ya sekretarieti,” alisema Masaga.

Wakati Masaga akieleza hayo, Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi CUF -Taifa, Yusuph Mbungiro alisema hadi juzi wanachama sita walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu tangu mchakato ulipoanza Julai 20.

“Tulianza mchakato huu Julai 20, mwisho Agosti 15 tutamaliza kuchukua na kurudisha fomu, hadi sasa wanachama sita wamejitokeza, kati yao wanawake watatu na wanaume watatu,” alisema Mbungiro.

Alitaja waliochukua fomu ni Sonia Magogo, Zainab Amiri, Thomas Malima, Mohamed Ngulangwa, QueenJulieth Lugembe na CUF, Mashaka Ngole.

Imeandikwa na Bakari Kiango, Jumanne Muyonga, Habel Chidawali na Lewis Mujemula