Mchopanga avunja rekodi Rorya

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka maarufu Mchopanga

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuwa miongoni mwa vigezo watakavyopimwa navyo ni ukusanyaji wa mapato.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikianza kushusha moto kwa halmashauri 85 zilizokusanya mapato chini ya malengo, huko Rorya wenyewe ni kama wameukwepa mtego huo, baada ya kukusanya mapato kwa asilimia 100.

Katika makusanyo ya mwaka wa fedha 2021/22, halmashauri ya Rorya imeivunja rekodi yake ya miaka 14 tangu mwaka wa fedha 2007/08, ambapo haikuwahi kufikia lengo la makusanyo.

Kuzibwa kwa mianya ya upotevu wa mapato na kusimamia ulipaji wa madeni kwa wafanyabiashara, ni miongoni mwa sababu zilizotajwa kufikiwa kwa hatua hiyo. Pia, mikakati ya Mkuu wa wilaya hiyo, Juma Chikoka maarufu Mchopanga, kuanzisha vyanzo vipya vya mapato vimechangia pakubwa.

Mwananchi limemtafuta Mchopanga kuzungumzia hatua hiyo ya kuvunja rekodi ya miaka 14 kwenye ukusanyaji mapato, ambapo amesema uwepo wa mapato ni jambo moja, lakini kuyakusanya ni jambo lingine.

“Mapato yapo lakini hayakuwa yanakusanywa yote, kwa hiyo tulichokifanya ni kuhakikisha hakana upotevu na tumeziba mianya yote, kuhakikisha kilichopo kinapatikana.

Lakini, sio kukusanya tu, tumetengeneza mazingira na miundombinu kuwawezesha wafanyabiashara kuzalisha na kufanya biashara kwenye mazingira salama na tulivu,” amesema.

Katika kufanikisha hilo, amesema mifumo ya makusanyo iliboreshwa ikiwemo kusitisha utaratibu wa kukusanya fedha kisha kuweka mifukoni, badala yake zilitumika mashine maalumu ‘Poss Machine’.

Kwa mujibu wa Chikoka, hatua nyingine iliyofanyika ni kudhibiti watu waliohodhi vyanzo vikiwanufaisha binafsi na hivyo mapato yote yalikwenda halmashauri.

“Watu walikuwa wanakusanya fedha wanaweka mfukoni kwa sasa tumeboresha ukikusanya hela inaonekana kwenye mfumo,” amesema.

Hatua nyingine iliyochukuliwa, amesema ni kuhakikisha wafanyabiashara wote waliokuwa wanadaiwa na halmashauri, wanalipa madeni yao kwa hiari ili kuongeza mapato.

“Nilikutana na wafanyabiasharam tukazungumza kwa busara wakakubali kulipa madeni yao, hii ndiyo siri ya kuongezeka kwa makusanyo,” amesema.

Si wafanyabisahara pekee, bali amesema hata vikundi vya wajasiriamali vilivyokopeshwa mikopo ya asilimia 10, alihakikisha vinarejesha ipasavyo na kwamba hilo lilifanikiwa.

Chikoka amesema katika mwaka huu wa fedha, dira iliyopo ni kuendelea kusimamia makusanyo, kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuziba mianya ya upotevu.

Ushirikiano baina yake na viongozi wengine wa halmashauri na baraza la madiwani, alitaja kuwa sababu nyingine iliyorahisisha kazi hiyo.

“Tutaendelea kuhakikisha tunakusanya mapato na kuhudumia wananchi vema, kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akituelekeza,” amesema.


Taarifa ya mapato ya miaka 14.

Mbali na makusanyo ya asilimia 100 katika mwaka wa fedha 2021/22, mwaka wa fedha 2020/21 ilikusanya asilimia 78, huku mwaka wa fedha 2019/20 ikikusanya asilimia 80.

Mwaka wa fedha 2018/19 ilikusanya asilimia 36, 2017/18 ilikusanya asilimia 39, 2016/17 asilimia 38, 2015/16 iliporomoka zaidi na kukusanya asilimia 21.

2014/15 ilikusanya asilimia 39, 2013/14 asilimia 32, 2012/13 asilimia 47, 2011/12 asilimia 41, mwaka 2010/11 asilimia 91, mwaka 2009/10 asilimia 43.

Kadhalika, katika mwaka wa fedha 2008/09 ilikusanya asilimia 36, 2007/08 ilikusanya asilimia 52.