Mchuano mwingine bungeni

Thursday January 14 2021
mchuanopic

Spika Job Ndugai

By

Dodoma. Ni mchuano mwingine bungeni. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana Bunge kutoa taarifa ya shughuli zitakazofanyika katika vikao vya kamati za Bunge ikiwemo uchaguzi wa wenyeviti na makamu wenyeviti wa kamati hizo.

Katika uchaguzi wa kamati hizo, wabunge wa CCM watachuana, huku wale wa upinzani wakitarajiwa kupambana kuwania kuongoza kamati za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za mitaa (Laac) ambazo kwa mujibu wa kanuni za Bunge lazima ziongozwe na wabunge wa upinzani.

Akizungumza na Mwananchi jana, Spika Job Ndugai alisema wabunge wa upinzani waliopo bungeni miongoni mwao ndio watakaoongoza kamati hizo.

“Anayeweza kuongoza kamati za PAC na Laac ni mbunge yeyote wa upinzani si kambi (ya upinzani)..., waliopo (wa upinzani) wataongoza na Bunge linaendelea kwa utaratibu wake maana wabunge wa upinzani wapo bungeni. Hakuna mkwamo wowote,” alisema Ndugai.

Wabunge wa upinzani waliopo bungeni ni sita; wanne wa ACT-Wazalendo, mmoja wa Chadema na mwingine wa CUF. Chadema wana nafasi nyingine 19 za wabunge wa viti maalumu ambao licha ya kuapishwa na Ndugai, chama hicho kilisema hakikuwapitisha na hivyo kuwafukuza uanachama. Hata hivyo, wanawake hao wakiongozwa na Halima Mdee wamekata rufaa baraza kuu la chama hicho kupinga uamuzi wa kufukuzwa na kuvuliwa nyadhifa zao.

Taarifa ya chombo hicho cha Dola iliyotolewa jana ilieleza kuwa vikao vya Bunge hilo la 12 vitaanza Jumatatu ya Januari 18 hadi 31 jijini Dodoma ikiwa ni vikao vyake vya kwanza tangu kuzinduliwa kwa Bunge hilo Novemba mwaka jana. Mbali na uchaguzi, shughuli nyingine zitakazofanyika bungeni ni mafunzo kwa wajumbe wa kamati za kudumu kuhusu majukumu na taratibu za uendeshaji wa kila kamati na mafunzo kuhusu Bunge mtandao na usalama wa mitandao ya kamati zote.

Advertisement

Shughuli nyingine ni kamati za kisekta kupokea maelezo ya wizara kuhusu muundo, majukumu ya taasisi pamoja na sera na sheria zinazosimamiwa na wizara hiyo.

Nyingine ni mafunzo kwa kamati za PAC, Laac, kamati za Uwekezaji na Mitaji kwa Umma (PIC) na Kamati ya Bajeti.

Taarifa hiyo ilisema mafunzo hayo yatahusu uchambuzi wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Msajili wa Hazina na namna bora ya kuhoji maofisa masuhuli.

Nyingine ni mafunzo kwa Kamati ya Sheria Ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo na uzoefu wa mabunge mengine ya nchi zinazofuata mfumo wa kibunge wa Jumuiya ya Madola.

Kwa upande wa kamati ya Bajeti, taarifa hiyo ilisema watapokea tathimini ya utekelezaji wa mpango wa pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano wa 2016/2017 hadi 2020/2021.

Pia ilisema kamati hiyo itapokea Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 hadi 2025/26 na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni utekelezaji wa bajeti ya Serikali pamoja na Sheria ya Fedha kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2020/2021.


Advertisement