MCL yazindua ‘Tunajenga Pamoja’ kuchochea ufanisi

Muktasari:

  •  Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Dk Wilfred Kiboro amezindua kaulimbiu mpya ya ndani ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) inayosema “Tunajenga Pamoja” ikilenga kuchochea ufanisi katika utendaji kazi.


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Dk Wilfred Kiboro amezindua kaulimbiu mpya ya ndani ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) inayosema “Tunajenga Pamoja” ikilenga kuchochea ufanisi katika utendaji kazi.

Dk Kiboro amefanya uzinduzi huo leo Juni 23 jijini hapa wakati wa kikao maalumu na wafanyakazi wa MCL ambayo ni mchapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti pamoja na kurasa zake katika mitandao ya kijamii.

Mbali na uzinduzi huo, mwenyekiti huyo amezungumza na wafanyakazi wa MCL na kuwataka kuongeza ufanisi katika kazi zao ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya ulimwengu katika utoaji wa habari.

Dk Kiboro amesema ni muhimu kutambua kwamba zama zimebadilika, vijana wengi hawapendi kusoma magazeti halisi, badala yake wanasoma kwenye mitandao ya kijamii kwa njia rahisi kupitia simu zao za mkononi.

Amewataka wafanyakazi kuweka mikakati ya kuwafikia wasomaji kwenye ulimwengu ili kuiwezesha kampuni kuongeza mapato kupitia huko, hasa kwa wakati huu ambao usomaji wa magazeti unazidi kuporomoka si tu Tanzania bali ulimwenguni kote.

“Lazima tuweke mikakati ya kufikia wasomaji kwenye mitandao ya kijamii. Tunawahusisha vipi watu wanaosoma maudhui yetu, hayo ndiyo mambo ya kujadili.

“Ningependa mkae pamoja na viongozi wenu mjadili, hii kampuni tunaiendesha namna gani. Mkifanikiwa katika hilo, mtaweza kuboresha maisha yenu ikiwemo kuongeza mishahara,” amesema Dk Kiboro.

Mwenyekiti huyo amesisitiza kwamba kampuni hiyo ni mali ya wafanyakazi na akawataka kuweka mikakati ya kuongeza mapato ili kuboresha maisha yao.

“Niwaombe, tuwe na azimio la kufukuza umasikini kwenye mifuko yenu. Na ili kufanikisha hilo, ni kuongeza bidii katika kazi,” amesema Dk Kiboro.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, Leonard Mususa amesema kuna fursa kubwa kwenye ulimwengu wa digitali, hivyo ni muhimu eneo hilo likapewa umuhimu mkubwa.

“Hatujaweza kutengeneza pesa kidigitali, wengi wanaosoma kidigitali wanapenda kusoma bure. Tunaweza kuwashawishi watangazaji kwamba wakiweka matangazo kwenye platform (kurasa) zetu watapata faida,” amesema Mususa.

Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema kampuni imepita katika kipindi kigumu kuanzia mwaka 2019 hadi 2021 kutokana na changamoto ya Uviko-19, jambo lililosababisha kampuni kuchukua hatua kadhaa, ikiwemo ya kupunguza wafanyakazi.

Hata hivyo, amesema sasa hali imeanza kuimarika, kampuni inatengeneza faida japokuwa bado ni ndogo. Amesisitiza kwamba jitihada zaidi zinahitajika ili kuongeza faida zaidi.

“Agosti mosi mwaka jana tuliingia kwenye change program (mpango wa mabadiliko), tulikutana na wafanyakazi na kuwauliza namna bora ya kufanya mabadiliko.

“Mwisho wa siku tukatoka na vipaumbele vinne ambavyo vimejikita katika lengo letu, watu wetu, utendaji kazi na bidhaa zetu,” amesema Machumu akisisitiza umuhimu wa shughuli zote kumlenga mlaji.