Meli nyingine iliyobeba korosho tani 15,800 yaondoka Mtwara

Muktasari:

  • Meli ya mwisho iliyobeba tani 15,800 za korosho msimu wa mwaka 2020/21 imeondoka leo Jumatano Juni 22, 2022 katika bandari ya Mtwara kuelekea nchini Vietnam.


Mtwara. Meli ya mwisho iliyobeba tani 15,800 za korosho msimu wa mwaka 2020/21 imeondoka leo Jumatano Juni 22, 2022 katika bandari ya Mtwara kuelekea nchini Vietnam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kaimu Meneja wa Bandari Mtwara, Norbert Kalembwe amesema katika msimu uliopita bandari ya mtwara ilisafirisha korosho zaidi ya tani 51,500.

“Hii ni meli ya mwisho kuelekea Vietnam kuondoka ambayo ilibeba tani 15,800 kwa sasa tunategemea meli ambayo itaingia wakati wowote ikiwa na viwatilifu aina ya Sulphur kwa ajili ya msimu huu” amesema Kalembwe

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Korosho Tanzania, Brigedia Generali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema meli iliyondoka leo imebeba korosho za Kampuni ya Sibatanza.

“Hii kampuni ilinunua korosho katika msimu uliopita tani 80,000 ambazo zilisafirishwa kwa awamu mbili  leo ndio wamekuja kumalizia awamu ya tatu ambapo kuondoka kwake kumetuongezea nafasi katika bandari yetu na inatupa moyo kuwa korosho zetu bado ni bora zinahitajika duniani” amesema  Mwanjile