Membe awakutanisha viongozi wa juu wa Serikali

Baadhi ya waombolezaji katika hafla ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe katika viwanja vya Karimjee

Muktasari:

  • Viongozi wa juu wa Serikali washiriki shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe.

Dar es Salaam. Serikali yote ipo hapa, hivi ndivyo inavyoweza kuelezwa kwa kile kinachoendelea katika viwanja vya Karimjee ambapo inafanyika shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe.

Membe ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Mtama alifariki asubuhi ya Mei 12, 2023 jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu katika hospitali ya Kairuki.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anayeongoza waombelezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwanadiplomasia mbobezi.

Mbali na kiongozi huyo wa juu wa Serikali shughuli hiyo ya kukuaga Membe imehudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Spika Mussa, Azan Zungu na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.

Wapo pia viongozi wa ulinzi na usalama akiwemo Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali Jacob Nkunda na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala.

Msiba huu umewakutanisha viongozi wa Serikali wastaafu akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange, mawaziri wa zamani, Stephen Wasira, William Ngeleja, Lazaro Nyalandu, Fenela Mukangara na Andrew Chenge.

Wanasiasa wa upinzani nao wamehudhuria shughuli hii ya kumuaga Membe akiwemo Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, mbunge wa zamani wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbles Lema na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo.