Meneja Ruwasa ‘aliangukia’ baraza la madiwani
Muktasari:
Kaimu Meneja wa Ruwasa wilayani Kaliuwa ameomba radhi Baraza la Madiwani baada ya kupita miezi mitatu tangu alipotamka kuwa hawajibiki kwenye baraza hilo.
Tabora. Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Mapambano Mashini ameliomba radhi Baraza la Madiwani la wilaya hiyo baada ya kumnyima ushirikiano kutokana na kauli yake yakuwa hawajibiki kwenye baraza hilo.
Januari mwaka huu katika kikao cha baraza hilo, Mapambano alilieleza kuwa hawajibiki kwao baada ya kutakiwa kuwasilisha rasimu ya bajeti ya Ruwasa ili waweze kuipitia.
Kutokana na kauli yake, baraza hilo lilimuamuru aendelee na majukumu yake na yeye kuondoka kisha kupitia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kaliua, Japhael Lufungija liliweka azimio la kutofanya naye kazi huku madiwani wakimlalamikia hana ushirikiano na hapokei simu wanapompigia.
Akiomba radhi Mei 5, 2023, Mapambano amewaahidi madiwani ushirikiano na kuwaomba radhi kwa kauli yake aliyoitoa.
"Waheshimiwa madiwani nawaomba radhi pamoja na baraza hili kwa kauli yangu iliyowakwaza na nawaomba ushirikiano wenu katika kuwahudumia wananchi"amesema
Nao madiwani wa halmashauri hiyo wamemsamehe na kumtaka kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza adha ya maji kwa wananchi, wakisema bado Kaliua hali ya upatikanaji wa maji ipo chini ya asilimia 50.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Japhael Lufungija amewashukuru madiwani kwa kusamehe na kuwataka kutoa ushirikiano kwa kaimu meneja huyo kwani wao wakiwa wawakilishi wa wananchi wana msaada mkubwa katika kuhakikisha miradi ya maji inatunzwa kwenye maeneo yao.
“Tunalo jukumu la kuhakikisha miradi ya maji iliyopo kwenye maeneo yetu inatunzwa lakini pia ile inayoendelea nayo inakuwa na ubora unaotakiwa"amesema
Amemtaka kuhakikisha fedha za miradi ya maji zinasimamiwa ipasavyo na miradi kuwa na ubora unaotakiwa ili idumu kwa muda mrefu.