Mfanyabiashara Kariakoo kizimbani akidaiwa kutishia kuua

Mfanyabiashara Kariakoo kizimbani akidaiwa kutishia kuua

Muktasari:

Adelard Lyakurwa (58),  mfanyabiashara katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam amefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Ilala akituhumiwa kutishia kumuua kwa bastola mfanyabiashara mwenzake, Valence Lekule.

Dar es Salaam. Adelard Lyakurwa (58),  mfanyabiashara katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam amefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Ilala akituhumiwa kutishia kumuua kwa bastola mfanyabiashara mwenzake, Valence Lekule.

Akisoma hati ya mashtaka jana Jumatano Mei 12, 2021 mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Martha Mpaze wakili wa Serikali, Aziza Mhina  amedai mshtakiwa huyo anakabiliwa  na shtaka  moja la kutishia kuua kwa kutumia bastola.

Amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 89 (2) (a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Mhina amedai Julai 30, 2020 maeneo ya Kariakoo mtaa Mbaruku na Swahili Wilaya ya Ilala akiwa na lengo la kuua, alimtishia Lekule kuwa atamuua kwa kutumia bastola wakati akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana na upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine ya kumsomea maelezo ya awali.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo Mpaze aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 2, 2021 na mshtakiwa alirejeshwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.