Mfanyakazi wa benki akatwa mkono na mumewe kisa wivu wa mapenzi

Mfanyakazi wa Benki akatwa mkono na muweke kisa wivu wa mapenzi

Muktasari:

  • Mfanyakazi wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi,  Debora Rwekwama (34) mkazi wa Bushushu mjini Shinyanga amekatwa mkono wa kushoto na mumewe, Jacob Mwajenga (35) ikidaiwa ni kutokana  na wivu wa mapenzi.

Shinyanga. Mkazi wa Bushushu mjini Shinyanga,  Debora Rwekwama (34) amekatwa mkono wa kushoto na mumewe, Jacob Mwajenga (35) ikidaiwa ni kutokana  na wivu wa mapenzi.

Kamanda wa  polisi mkoani Shinyanga,  George Kyando amesema tukio hilo limetokea Septemba 9, 2021 mtaa wa Bushushu manispaa ya Shinyanga.

Amesema mwanaume huyo alimkata mkono Debora baada ya mwanamke huyo kuzimia kwa kipigo.

"Inadaiwa mwanaume huyo mchana alikwenda benki (inayodaiwa mkewe kufanya kazi)hakumkuta mkewe lakini alikuta mkoba wake katika ofisi   na aliporejea alitaka kuanzisha vurugu lakini wakamshauri ugomvi wao wakaumalize nyumbani."

"Walipofika nyumbani waliendelea na ugomvi na alimpiga sana mkewe hadi akazirai. Alichukua kisu na kumkata mkono inaonekana zilitoka damu nyingi. Mkewe akiwa amezimia huyu mwanaume alimbeba na kumpakia kwenye gari  na kwenda wilayani Kahama katika kituo cha polisi na kuripoti kuwa  amepata ajali. Kwa sababu Debora  alikuwa hawezi kuongea  hawakumhoji huhu mwanaume walimpa PF 3 ili aweze  kutibiwa lakini hawakujua kama ni mke wake."

"Alipomfikisha hospitali madaktari walifanya uchunguzi wao na kugundua kuwa hajapata ajali bali amepigwa na walitoa taarifa polisi wilaya ya Kahama ambao walimkamata mhusika ambaye shughuli yake ni kuongoza watalii huko Arusha na kutokana na changamoto ya corona alikuwa nyumbani tu,  nadhani ndio wivu ulipoanzia hapo, "amesema Kyando.

Amesema Debora amelazwa  hospitali ya Wilaya ya Kahama na hali yake ni mbaya, " tunamshikilia mtuhumiwa  kwa ajili ya uchunguzi zaidi."