Mfugaji adaiwa kumpiga risasi mkulima

Kamanda wa Polisi Mkoa wa manyara, RPC George Katabazi akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Mohamed Hamad 

Muktasari:

  • Majeruhi ambaye ni mkulima, alikuwa akijaribu kuondoa ng'ombe waliokuwa wameingia shambani kwake na kufanya uharibifu wa mazao yalikuwa yamelimwa shambani humo, ndipo alipotokea mfugaji huyo na kuzozana.

Simanjiro. Mkulima Walter Kaaya (34) mkazi wa Simanjiro mkoani Manyara amenusurika kifo baada ya kudaiwa kupigwa risasi na mfugaji Paulo Laizer (43) baada ya kutokea mzozo uliotokana na ng’ombe kuvamia shamba na kuharibu mazao.

Inadaiwa kuwa Kaaya alikuwa akijaribu kuwaondoa ng’ombe hao ambao alikuwa akiondoa mifugo hiyo ili kuepusha uharibifu kwenye shamba lake la ekari 200, na lenye mazao mbalimbali kama vile mahindi na maharage.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Juni 2, 2023 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara (RPC), George Katabazi amesema wakati mkulima huyo anawaondoa mifugo hao, mtuhumiwa alifika na kuibua mzozo na kuchukua silaha yake aina ya bastola na kumpiga risasi begani.

"Majeruhi amewahishwa Hospitali ya KCMC Moshi kwa matibabu zaidi japo baada ya tukio, mtuhumiwa alitoroka. Hata hivyo, Jeshi la Polisi tulianza jitihada za kumtafuta na kufanikiwa kumkamata alipokuwa kajificha katika Kijiji cha Nyumba ya Mungu wilayani ya Simanjiro Mkoa wa Manyara," amesema.

Kamanda Katabazi amesema kitendo hicho ni kujichukulia sheria mkononi na kwamba angetumia taratibu za kisheria kwa kutumia viongozi na hata angefika polisi hayo yote yasingeweza kujitokeza.

"Alifanya maamuzi ya kujichukulia sheria mikononi na hakukuwa na sababu yoyote ya kumjeruhi... angetumia tu taratibu, kuna uongozi hapo, Polisi wapo lakini yeye akaamua eti kwa sababu ana silaha na kiburi tu cha mali akaamua kutumia nguvu," amesema RPC Katabazi na kuongeza;

"Wananchi walifikiri kwamba kwa kuwa mtuhumiwa ni mtu mwenye mifugo na mwenye fedha ni vigumu kukamatika lakini sisi Jeshi la Polisi kwa weledi wetu na maadili tulimkamata na kumtia mbaroni na sasa tunafanya utaratibu wa kumfikisha mahakamani."

Kuhusu suala la uharibufu wa mali Kamanda Katabazi amesema hilo nalo litazingatiwa ingawa tatizo kubwa hapo ni kujeruhi.

"Kosa kubwa hapo ni kujeruhi na ikizingatiwa mahali alipojeruhiwa huyu mtu angeweza hata kupoteza maisha, tunashukuru Mungu anaendelea vizuri na matibabu hapo KCMC maana kabla hatujaangalia suala la uharibifu wa mazao, uhai wa binadamu unapewa kipaumbele," amesisitiza RPC Katabazi

Amesema kitendo hicho ni matumizi mabaya ya silaha ambayo anaimiliki kwa mujibu wa sheria: "Mtu akiona kuwa ana silaha hapaswi kujichukulia sheria mkononi, asijione kwamba anaweza kufanya lolote hapana...tunataka wananchi wazingatie sheria hata kama wanamiliki hizo silaha watumie tu lakini sio kinyume cha sheria."