Mfumo malipo ya tozo, vibali usafirishaji mbao wakwamisha malori

Muktasari:

  • Zaidi ya malori mia mbili yaliyobeba mbao mkoani Njombe, yamekwama kuondoka kwa zaidi ya wiki moja, kwa kile kinachodaiwa ‘kukwama kwa mfumo’ wa malipo ya tozo za vibali katika usafirishaji wa mazao hayo ya misitu.

Njombe. Zaidi ya malori mia mbili yaliyobeba mbao mkoani Njombe, yamekwama kuondoka kwa zaidi ya wiki moja, kwa kile kinachodaiwa ‘kukwama kwa mfumo’ wa malipo ya tozo za vibali katika usafirishaji wa mazao hayo ya misitu.

Wakitoa malalamiko yao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, leo Alhamisi Septemba 21, 2023; baadhi ya wafanyabiashara wa mbao, wamesema hi ini mara ya pili kwa tatizo hilo kujitokeza ambapo mara ya kwanza ilikua mwezi July mwaka huu.

Kwa mujibu wa malalamiko yao, licha kulipia tozo hizo kwa mtandao, pale wanapofuatilia vibari ndipo shida huanza, kwani huambiwa na mamlaka husika kuwa “mfumo unasumbua,” jambo ambalo husababisha washindwe kushafirisha shehena hiyo ya mbao.

Wafanyabiashara hao, wamemueleza RC huyo kuwa ucheleweshaji huo, unawaghari katika kufanya marejesho ya mikopo waliyochukua, lakini pia inawapunguzia uaminifu kwa wateja wao.

Kwa nyakati tofauti, Sophia Raymond na Subira Kyando ambao ni sehemu ya wafanyabiashara hao, wamemuomba RC Mtaka kuwasaidia katika kupunguza vituo vya ukaguzi wa mazao ya misitu, wakidai siyo tu vimekuwa vikileta usumbufu, lakini pia vinachukua ambao ungetumika safarini.

"Hii faini ambayo maliasili wamekuwa wakiwapiga madereva sababu ya kuruka kituo bila kukaguliwa ni uonevu, madereva wengine ni wageni hivyo kuwe na vituo vichache vitakavyotambulika kwa urahisi," amesema Sophia.

Kwa upande wake, Wakala wa Misitu mkoani humo, Audatus Kashamakula, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kudai kuwa imetokana na kusimama kwa mifumo wa utozaji kodi wa Wizara ya Fedha, jambo ambalo lipo nje ya uwezo wao.

Amesema wamekuwa wakijitahidi kutoa huduma hata muda wa ziada ili kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika utoaji wa vibali.

"Nipende kuwaomba radhi wadau wetu wa mazao ya misitu, wasafirishaji na madereva, kwa hili ambalo limetokea. Tulifanyia kazi, changamoto zote ambazo zimetokea hasa mfumo ambao ulikuwa haujakaa sawa," amesema Kashamakula.

RC Mtaka yeye ameziomba ameziomba wizara zinazohusika, kushughulikia tatizo hilo haraka ili kunusuru mapato ya mkoa huo ambapo zaidi ya asilimia sabini ya mampato ya ndani ya mkoa huo, yanategemea mazao hayo.

“Uchumi wa Mkoa wa Njombe kwa zaidi ya asilimia sabini, unategemea mazao yatokanayo na misitu hivyo lazima kuwepo na usimamizi utakaoweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara wa mazao haya, hivyo tunao wajibu wa kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya biashara kuliko kuwaza kukusanya tu,” amesema.