Mfumo mpya wa kutuma fedha kwa simu kuanza Julai

Mfumo mpya wa kutuma fedha kwa simu kuanza Julai

Muktasari:

  • Utekelezaji wa mfumo huo ulipangwa kuanza Juni, mwaka jana lakini kutokana na maambukizi ya virusi vya corona haukuanza

Dar es Salaam. Kuanzia Julai Watanzania wataweza kutuma fedha haraka kwa watu waliopo kwenye orodha zao za mawasiliano ya simu bila kutafuta namba za majina husika.

Hiyo itawezekana kwa sababu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itazindua mfumo wake wa Malipo ya Haraka (Tips).

Tips itahamasisha miunganisho ya huduma za fedha za kidigitali yakiwamo malipo kwa watoa huduma kwa gharama nafuu na zenye ulinzi.

Mfumo huo utafanya kazi kwa njia ambayo malipo yote ya kidigitali, yakiwamo ya miamala ya simu kama Airtel Money, Tigo Pesa, M-Pesa, HaloPesa, EzyPesa na T-Pesa, itakayounganishwa katika jukwaa moja.

Kwa hiyo, mtu anayetaka kutuma fedha atahitajika kuwa na jina la mtu anayetaka kutumiwa kabla ya kutuma.

Mfumo huo unaelezwa utarahisisha utumaji wa fedha na kupunguza gharama.

Awali, mfumo huo ulitarajiwa kuanza kufanya kazi Desemba mwaka jana, lakini Mkurugenzi mifumo ya malipo wa BoT, Bernard Dadi alisema waliamua kuuboresha kwa kuubadilisha na kuujenga upya.

“Mpango huo unatarajiwa kuwa tayari katika awamu ya kwanza Julai mwaka huu,” alisema Dadi.

Awamu hiyo itahusu biashara ya mtu kwa mtu.

Dadi alisema baada ya awamu hiyo ya kwanza, kutakuwa na awamu ya pili, ya tatu na mwisho awamu ya nne itakayohusisha ulipaji wa kodi na malipo ya jumla na mengineyo yatakayojitokeza katika masoko.

Pia, alisema, utekelezaji wake pia ulipangwa kuanza Juni, mwaka jana lakini kutokana na maambukizi ya virusi vya corona ulihifadhiwa kwanza.

BoT iliisitisha timu liyokuwa ikitekeleza mradi huo kutokana na maambukizi ya corona na kuanzisha timu nyingine.

Hata hivyo, baada ya kuundwa kwa timu nyingine mfumo huo haukuweza kuzinduliwa kwa muda uliotarajiwa yaani Juni na ulisogezwa hadi mwisho wa mwaka jana.

Maandalizi ya matumizi ya mfumo huo ambayo yatafanyakazi kupitia kadi za malipo, benki za simu, uchumi wa kidijitali na benki za intaneti, yalianza kufanyika tangu Juni 2018. Na matumizi hayo yalipangwa kufanyika kwa bidhaa za fedha na kwa watoa huduma.

Matumizi ya mfumo huo yanalenga kupunguza matumizi ya fedha tasilimu katika malipo na katika uchumi.