Mgogoro aliyechonga kifimbo cha Nyerere kuchimbiwa makaburi mawili
Muktasari:
- Mzozo wa familia juu ya maziko ya Mzee Omary Mwariko, ambaye alichonga kifimbo cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, umechukua sura mpya baada ya upande mmoja wa familia kukataa mzee huyo kuzikwa nyumbani kwake alikozaliwa huku wakilazimika kuchimba makaburi mawili, moja likiachwa wazi.
Moshi. Omary Mwariko ambaye anatajwa kuwa ndiye aliyochonga kifimbo cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amezikwa leo jioni katika makaburi ya Manyema, yaliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya kuibuka mvutano mkali ndani ya familia kwamba mzee huyo azikwe wapi.
Mzee huyo ambaye ni mwanasiasa, msanii na mwana utamaduni alifariki jana jumapili katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini, KCMC alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Jana Januari 23, upande mmoja wa familia walichimba kaburi kwenye nyumba yake iliyopo eneo la Njoro, Kata ya Miembeni huku mmoja wa ndugu wa mzee huyo akikataa mzee huyo kuzikwa katika eneo hilo licha ya kaburi kuchimbwa jambo ambalo lilizua taharuki kuanzia asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni huku upande mmoja ukikubali yaishe na kwenda kuzika katika makaburi ya umma.
Hata hivyo ndugu jamaa na marafiki waliokwepo katika eneo hilo kwa ajili ya maombolezo walilazimika kuondoka katika eneo hilo kutokana na mzozo mkali uliokuwepo katika familia hiyo huku wakiacha kaburi likiwa wazi mpaka usiku huu.
Akizungumza na Mwananchi Digital, mtoto wa kwanza wa mzee huyo, Kennedy Mwariko amesema baba yake huyo aliwahi kusema azikwe Njoro kwenye eneo alilokuwa akiishi na wazazi wake lakini kutokana na mzozo wa familia ikawalazimu kwenda kuzika katika makaburi ya umma.
"Mzee wangu alitaka azikiwe Njoro alikokuwa akiishi na baba na mama yake, maana baba yetu alizaliwa Moshi na amesoma Moshi mpaka alipofariki jana, kwa hiyo alitaka azikiwe kwenye eneo hilo lakini kwenye mazishi pakatokea tatizo hivyo tukaona kuliko tulumbane bora tumpumzishe tu mzee wetu," amesema.
"Licha ya kwamba kule nyumbani Njoro kulikuwa kumeshachimbwa kaburi kwa ajili ya kumpumzisha baba na kukaibuka mzozo, ikatupelekea kukaa mpaka jioni hii bila kumzika baba yetu. Kwa hiyo imetulazimu jioni hii tutafute eneo jingine ambalo atazikwa muda huu ambapo ni kwenye makaburi ya jumuiya, hivyo tumempumzisha baba yetu mpendwa," amefafanua.
Kuhusu kaburi moja kuchimbwa na kuachwa wazi amesema, "Tutakaa tuangalie jinsi ya kulifukia lile kaburi la mwanzo maana likibaki hivyo linaweza likaleta matatizo makubwa kwa hiyo tukishamsitiri baba yetu jioni hii tutakaa tuangalie namna ya kulifunika lile kaburi la mwanzo."
Mmoja wa wananchi wa Mji wa Moshi, Amani Tesha amesema kwa desturi na mila za Kichaga kuacha kaburi wazi bila kuzika ni jambo hatari na kwa tafsiri yake mtu mwingine wa familia hiyo anaweza kufa.
"Kwa mila za Kichaga kuacha kaburi wazi ni jambo baya kwa maana yake likiendelea kuwa wazi linaweza kuvuta mti mwingine au likamaliza familia nzima, labda cha kufanya wakate mgomba watumbukize ndani ya kaburi, wakifanya hivyo haliwezi kuleta madhara."
Mzee huyo ambaye ameacha watoto zaidi ya 13 alikuwa ni kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya mwaka 2005 kuwania nafasi ya urais lakini pia hotuba zake zilikuwa zikiwavutia wana CCM kutokana na vichekesho vyake.
Mwaka 2015 wakati akiomba kura kwa Wana CCM katika kura za maoni kugombea ubunge Jimbo la Moshi Mjini moja ya ahadi zake ni kuweka pazia kuuzunguka Mlima Kilimanjaro kuzuia Wakenya kutangaza mlima huo ni wa kwao.