Miaka 60 ya WWF imeleta mapinduzi katika uhifadhi wa mazingira na wanyamapori

Thursday June 03 2021
toleo maalumpic

Tembo aliyewekewa kola ya kufuatilia mwenendo wake katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa msaada wa WWF.

Mwaka 1961, nchini Uingereza habari za ujangiri na uharibifu wa mazingira kutoka mataifa ya Afrika Mashariki zilitanda magazetini kwa wiki kadhaa mfululizo.

Hili lilisababisha mfanyabiashara Victor Stolan kuwatafuta rafiki zake wachache wadau wa mazingira na kuwashawishi wafanye kitu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nature Conservancy wakati huo Max Nicholson alilipokea wazo hilo na akaona hii ni fursa ya kuusaidia Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (International Union for Conservation of Nature IUCN) ambao wakati huo ulikuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha kusaidia katika kazi zake za uhifadhi.

Akaona iko haja ya kuanzisha mfuko wa kimataifa ambao utasidia shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira duniani bila kuwa na mipaka wala masharti magumu.

Hatimaye likasainiwa azimio lililokuja kujulikana kama Azimio la Morges (Morges Manifesto), lililopelekea kuanzishwa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Duniani, World Wildlife Fund (WWF) na Mwana Mfalme wa Uholanzi Bernhard akawa Raisi wa kwanza wa mfuko huu.

toleo maalumpic

Tembo aliyewekewa kola ya kufuatilia mwenendo wake katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa msaada wa WWF.

Advertisement

Miaka 60 baadaye WWF imekuwa moja ya mashirika yasiyo ya kiserikali makubwa katika uhifadhi wa mazingira huku ikiwa na ofisi katika nchi zaidi ya 100 duniani na watu zaidi ya milioni tano wakisaidia kutafuta rasilimali ili kuwezesha uhifadhi.

Hakika hii imekuwa kubwa kuliko ndoto waliyokuwa nayo waanzilishi wa mfuko huo mwaka 1961.Miaka 60 ni umri wa mtu mzima haswa ambaye hapana shaka atakuwa nayo mengi ya kusimulia katika safari yake ya maisha, hii ni sawa pia kwa WWF ambayo katika kipindi cha uwepo wake imefanikiwa kufanya mengi katika uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha kuwa dunia inakuwa salama kwa binadamu na viumbe wengine kuishi.

Kama ilivyo kwa mwanadamu, safari ya WWF pia imekuwa na mafanikio na changanoto mbalimbali ndani ya miaka yake 60, hata hivyo nafasi hii ni ya kusherehekea mafanikio kwani changamoto zimetumika kama funzo katika kuyafikia mafanikio makubwa yanayoonekana leo hii.

toleomaalummpicc

Mkurugenzi Mkaazi wa WWF Tanzania, Dk Amani Ngusaru akizindua mtambo wa kuzalisha barafu uliotolewa na WWF kwa wakazi wa kisiwa cha Songosongo ili kudhibiti upotevu wa mazao ya bahari kisiwani humo.

Ikianza kama mfuko wa uwezeshaji wa kifedha kwa mashirika na mataifa mbalimbali katika uhifadhi wa wanyamapori na makazi yao, mwaka 1986 WWF ilibadili jina na kuwa Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (World Wide Fund for Nature) hii ikilenga kuonyesha muktadha wa kazi zake kwa ujumla ambazo zinalenga zaidi ya wanyamapori na kujumuisha maeneo mengine mtambuka kama misitu, maji baridi, bahari, chakula, nishati na mabadiliko ya tabia nchi, lakini muhimu kabisa binadamu na uhusiano wake na maeneo haya.

Utekelezaji katika maeneo haya umewezeshwa na sera imara, ushirikiano baina ya wadau mbalimbali, matokeo ya kisayansi bila kusahau uwezeshaji wa kifedha na biashara.

WWF imekuwa na maono ya kuwezesha kutengeneza mazingira ambayo binadamu ataishi na viumbe wengine duniani kwa maelewano huku ikiazimia kufikia maono haya kwa kuhifadhi bioanuai ya dunia, kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na endelevu, kupunguza uchafuzi wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu ya maliasili.

WWF Tanzania

Hali ya sintofahamu juu ya ujangili Afrika Mashariki ambayo ndiyo haswa chimbuko la WWF ililazimu kuanzishwa kwa shughuli za WWF hapa nchini mapema tu tangu miaka ya mwanzoni ya sitini, wakati huo utekelezaji ukisimamiwa kutoka makao makuu Uswisi. Miradi ya kuhamasisha uhifadhi wa faru ilikuwa ya mwanzo kabisa hapa nchini.

toleomaalumpinyiinyinginee

Upandaji wa miti ni sehemu muhimu ya kurejesha mfumo ikolojia na uoto asili.

Muhimu zaidi ni mchango wa WWF katika kuanzishwa kwa chuo cha kwanza cha usimamizi wa wanyamapori Afrika (Mweka). WWF imeendelea kuwa mjumbe wa bodi ya chuo hiki tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990 WWF Tanzania ikapata nafasi ya kuwa na ofisi na kuweza kutekeleza na kusimamia miradi yake kutokea hapa hapa nchini. Ikiongozwa na mpango mkakati wa miaka mitano mitano, WWF ofisi ya Tanzania imeendelea kuyafanyia kazi maono ya waasisi wake katika maeneo muhimu ya wanyamapori, misitu, maji baridi, bahari, nishati na mabadiliko tabia nchi.

Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huku mdau mkubwa akiwa Serikali na taasisi zake, wanajamii katika maeneo ya utekelezaji na asasi za kijamii na za kimataifa zenye mtazamo kama wa WWF, mafanikio makubwa yameonekana katika uhifadhi wa mazingira.

WWF katika uhifadhi wa bahari

WWF imekuwa na mchango mkubwa katika uanzishwaji wa vikundi vya kijamii vya usimamizi wa fukwe za bahari na mazao yake (Beach Management Units – BMUs) katika maeneo muhimu ya utekelezaji ya ukanda wa Bahari ya Hindi kuanzia Dar es Salaam mpaka Mtwara. Jumla ya BMUs 70 zimeanzishwa.

Hizi zikiwa na jukumu la kuhakikisha maliasili za bahari zinalindwa kwa kufanya doria, kukusanya takwimu kitaalamu lakini pia kuhakikisha wananchi wananufaika ipasavyo na maliasili za bahari zilizo katika maeneo yao.

Hizi zimekuwa na mafanikio makubwa. Thomas Chale mmoja wa maofisa aliyekuwepo wakati WWF ikiingia Pwani kuanzisha anasimulia safari ambayo haikuwa rahisi.

“Tulipofika Pwani kuutambulisha mradi hatukukubalika kabisa, wengi waliambizana na kuamini kuwa tumekwenda kuiuza bahari yao na sasa hawataruhusiwa tena kuendelea na shughuli zao za uvuvi. Walitutupia mawe na kutufukuza, lakini hatukukata tamaa na kwa kweli Serikali ilitusaidia sana kupeleka elimu sahihi kwa jamii hizi za wavuvi, baadaye kidogo kidogo mitazamo yao ikabadilika na sasa tunapata ushirikaino mkubwa mno kutoka kwa wanajamii na viongozi. Sasa wamekuwa walinzi na wasimamizi wa rasilimali zao, hata mradi ukiondoka leo hatuna wasiwasi kuwa wataendelea kwa weledi mkubwa”

Miaka michache tu iliyopita Tanzania ilikuwa nchi pekee ambayo ina changamoto kubwa ya uvuvi haramu hasa wa kutumia milipuko. Jitihada kubwa zilifanywa na WWF na wadau wengine ambapo elimu ilitolewa bila kukoma huku Serikali na vikundi vya ulinzi vya wanajamii wakiwezeshwa kufuatilia na kuwafikisha katika vyombo husika wahalifu.

Haikuwa safari rahisi, ilikumbana na vikwazo vingi lakini hatimaye ilifanikiwa na sasa takwimu zinaonyesha hakuna kabisa uvuvi wa milipuko katika sehemu nyingi na maeneo machache kukiwa na milipuko kwa kiasi cha asilimia moja tu kulinganisha na miaka saba iliyopita.

Ili kupunguza utegemezi wa bahari kwa maisha yao, wanajamii za uvuvi baada ya kupata elimu waliona ni vyema kuwa na shughuli nyingine za kuwaingizia kipato. Changamoto kubwa ikawa ni namna ya kupata mitaji, hapo ndipo WWF ilipowapelekea wazo la kuanzisha vikundi vya kijamii vya kiuchumi (Vicoba).

Mwitikio ulikuwa mkubwa na mara moja wanawake kwa wanaume wakajitokeza kujiunga katika vikundi hivi, wakapatiwa elimu ya uendeshaji na baada ya hapo yaliyobaki ni historia. Jumla ya Vicoba 363 vimeanzishwa na hakika maisha ya wananchi wanachama wa Vicoba yamebadilika kabisa.

Salha Rubama amekuwa mwanachama wa Vicoba tangu mwaka 2007 na sasa anamiliki duka lenye thamani ya zaidi ya Sh20 milioni. Wengi wana hadithi za kusisimua juu ya maisha yao yalivyobadilika kutokana na mfumo huu wa Vicoba.

WWF katika uhifadhi wa misitu

Mradi wa uhifadhi wa misitu umekuwa moja ya miradi mikubwa na ya muda mrefu inayotekelezwa na WWF nchini. Chini ya mradi huu kumekuwa na mafanikio makubwa katika uhifadhi wa misitu na urejeshaji wa uoto asilia.

Kazi kubwa imefanyika katika kuanzisha misitu ya vijiji ambayo inasimamiwa na wanavijiji na kunufaisha vijiji husika haswa katika mahitaji ya kijamii kama afya ambapo zahanati kadhaa zimewezeshwa vifaa.

Kijijini Nanjilinji mamilioni ya pesa yaliyopatikana kutokana na kuuza magogo yaliyotokana na uhifadhi wa misitu ya kijiji wamefanikiwa kujenga ofisi nzuri ya Serikali, madarasa ya shule ya kijiji na hata kuboresha huduma za afya.

Jumla ya hekta 457.946 katika vijiji 45 vya eneo la mradi zimeingia kwenye misitu hifadhi ya vijiji na hii imefanikisha kupatikana kwa mamilioni ya pesa ambayo yamesaidia kuinua maisha ya wanajamii katika vijiji hivi.

WWF pia imesaidia kuwatafutia masoko wanajamii wa vijiji hivi na wawekezaji kwa ajili ya kusaidia maendeleeo yao.

Mashine za kisasa za kuchakata magogo na mazao yake imekuwa eneo jingine ambalo WWF imewezesha kwa kiasi kikubwa. Juhudi hizi zimeenda sambamba na kuotesha miti ili kurejesha uoto wa asili katika maeneo mbalimbali ya miradi huku zaidi ya miche laki moja na nusu ikiwa imepandwa maeneo mbalimbali hapa nchini.

WWF imekuwa pia mdau mkubwa katika kuisaidia Serikali kutekeleza lengo la kuhifadhi hekta milioni 5.2 kama sehemu ya mchango wa Tanzania kurejesha uoto wa asili kwa hekta milioni 100 barani Afrika.

Kwa namna ya pekee WWF imefanikiwa kusaidia kurejeshwa kwa mti aina ya Erythrina schliebenii ambao uliripotiwa kutoweka na baadaye kugundulika miche chini ya 50 mwaka 2012 maeneo ya Kilwa.

Mti huu asili yake ni Tanzania pekee, na kwa jitihada za WWF na wadau sasa miche zaidi ya 29,090 imeoteshwa na hivyo kupatikana kwa matumaini kuwa mti huu sasa utarejea na kutoka kwenye orodha nyekundu ya shirika la International Union for Conservation of Nature (IUCN).

WWF katika uhifadhi wa wanyamapori

Mara nyingi tunaposikia WWF wengi wetu huwaza zaidi wanyamapori kama tembo na faru, hii ni kwa kuwa eneo hili limekuwa moja ya maeneo muhimu sana kwa WWF na utekelezaji wake umeendelea kwa miaka kadhaa sasa.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961, WWF imekuwa ikiwekeza katika uhifadhi wa wanyama hawa adhimu kabisa hapa nchini. Kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu, uharibifu wa mazingira na hata uhalifu dhidi ya wanyamapori kama ujangili, baadhi ya wanyamapori kama Tembo, Faru na Simba wametatizika sana na kupelekea wengi kupoteza makazi yao na hata kuuwawa.

Lakini zaidi sana hali hii imesababisha kwa kiasi kikubwa migogoro kati ya binadamu na wanyama. Hii ilitoa msukumo kwa WWF kuwekeza nguvu zake katika kusaidia kutatua changamoto hizi. Kwa hakika yapo mengi ya mafanikio na mkono wa WWF umeonekana katika maeneo muhimu ya hifadhi ya wanyamapori katika Pori la Akiba la Selous na Ekolojia ya Mikumi Selous na ukanda wa Kaskazini maeneo ya Serengeti, Mkomazi na Manyara.Jitihada hizi zimeeenda pia katika kutoa elimu na kuwezesha usimamizi na utungaji wa sera, utafiti na uwezeshaji wa vitendea kazi kwa timu za wahifadhi.

Kwa namna ya pekee WWF kwa kushirikiana na wadau wamewezesha kuanzishwa kwa jumuia za uhifadhi (Wildlife Management Areas) ambazo zimekuwa za msaada mkubwa wa kulinda na kuhifadhi wanyamapori.

Ripoti za hivi karibuni kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) zimeonyesha sasa kuna ongezeko lenye kuleta matumaini la tembo na faru weusi kutoka tembo 43,000 mwaka 2015 mpaka 51,000 mwaka 2019 na faru 100 mpaka 190 mwaka 2019.

WWF katika uhifadhi wa maji baridi

Mradi mwingine muhimu ambao WWF imekuwa ikitekeleza hapa nchini ni wa uhifadhi katika mabonde muhimu ya Rufiji, Ziwa Viktoria na Kilombero. Chini ya mradi huu tumeshuhudia uanzishwa wa jumuia za watumia maji (Water Users Associations) zipatazo 44 mkoani Mara, Iringa na Mbeya ambazo zimesaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na kufufua vile ambavyo vilikwisha haribiwa kutokana na shughuli mbalimbali haswa kilimo na ufugaji.

Jumla ya vyanzo 126 vimehifadhiwa katika kipindi cha miaka mitano huku miti zaidi ya 50,000 ikipandwa. Mipango bora ya matumizi ya ardhi limekuwa ni eneo jingine ambalo WWF imesaidia hasa Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini kwa kushirikiana na Serikali za wilaya na vijiji.

Mpaka sasa vijiji 11 vimehusika katika mpango huu na wananchi wake zaidi ya 2,997 wmepatiwa umiliki halali wa ardhi miongoni mwao asilimia 45 wakiwa wanawake.

WWF imekuwa pia mjumbe wa tume maalumu chini ya ofisi ya Makamu wa Rais kuangalia chanzo na suluhu ya kukauka kwa mto Ruaha Mkuu katika miaka ya karibuni. Kwa hakika mengi yamefanyika na mafanikio makubwa yameonekana na maisha ya watu wengi yameguswa. Salma Chatto ni mmoja wa watu hao wenye hadithi ya kusisimua.

Yeye sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya pili nchini Vietnam. Akiwa mzaliwa wa kisiwa cha Mafia miaka kadhaa nyuma, watoto wa kike hawakuwa wakisoma, wengi walishindwa kumaliza hata darasa la saba. Akiwa madarasa ya awali WWF walitambulisha mradi wa kuwasaidia watoto wa kike kielimu. Na ndipo alipopata nafasi ya kuiona ndoto yake ikitimia.

“Kwa miaka hiyo sikutegemea kuwa ningemaliza hata darasa la saba, nilijitahidi na hatimaye kutoka shule yetu pekee wakati huo kisiwani Mafia nilikuwa mwanafunzi pekee niliyefaulu na kujiunga na kidato cha kwanza. Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa mwanasayansi wa bahari ili niweze kuwasaidia ndugu zangu kisiwani humo. Mimi sasa ni mwalimu katika chuo cha Uvuvi Mikindani. Isingekuwa WWF sijui ningekuwa wapi sasa. Wapo wenzangu wengine zaidi ya 50 ambao tumenufaika na mradi huu. Ninajivunia kuwa sehemu ya familia ya WWF na hakika wamenikomboa”,

Mkurugenzi Mkaazi wa WWF Tanzania Dk Amani Ngusaru anasema haya yamewezekana kwa ushirikiano mkubwa wa wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, asasi za kijamii, mashirika mengine ya kimataifa na jamii ambazo WWF imekuwa ikitekeleza miradi yake.

Mashirikiano haya ni matumaini yangu kuwa yataendelea kudumishwa kwani kwa hakika yako mengi yanayohitaji kufanywa tena ndani ya miaka kumi tu, haya ni makubwa kuliko yale yaliyofanyika ndani ya miaka sitini.

Ripoti ya Living Planet ya mwaka 2020 inaeleza kuwa mbili ya tatu ya wanyamapori wametoweka duniani ndani ya miaka 50 tu na hii ni tishio kwa upatikanaji wa chakula, maji, mabadiliko ya tabianchi na afya zetu na uhai kwa ujumla.

Magonjwa kama Covid-19 yanayodaiwa kutokana na mabadiliko katika matumizi yetu ya ardhi, uharibifu wa mazingira kama kukata miti na biashara haramu za wanyamapori ni ushahidi tosha kuwa shughuli zetu zisizo endelevu zinaipeleka baioanuai ya dunia katika ukingo wa hatari.

Hii itusaidie katika kutafakari upya uhusiano wetu na mazingira na kwa pamoja kuweka mikakati na kufanya maamuzi muhimu kwa haraka ili kuiokoa dunia. “Tunaweza kufanya hili na kufanikiwa pamoja.”

Advertisement