Miamala ya fedha kwa njia ya simu yaongeza pato la Taifa

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema thamani ya miamala ya fedha kwa njia ya simu imechangia kuongezeka kwa pato la Taifa kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 66.


Arusha. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema thamani ya miamala ya fedha kwa njia ya simu imechangia kuongezeka kwa pato la Taifa kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 66.

Dk Nchemba ametoa kauli hiyo leo Juni 23, 2022 wakati akifungua kwa njia ya mtandao mkutano wa 10 ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Jumuiya ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI) ulioshirikisha viongozi wa jumuiya hiyo ukanda wa Afrika (AfPI) unaofanyika jijini Arusha.

Amesema kuwa thamani ya miamala hiyo imeongezeka kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 66 mwaka jana na kuwa watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu ilikuwa milioni 35.3 hadi mwezi Desemba mwaka jana sawa na asilimia 61 ya watu wote nchini.

"Kuanzishwa kwa huduma hizi za kifedha kwa njia ya simu, pamoja na huduma za benki kwa wakala na benki kwa njia ya simu, kuliongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijijini," amesema.

Amesema kupitia mkutano huo washiriki hao watajadiliana na kubadilishana uzoefu juu ya namna sekta hiyo itakuwa ya kidijitali zaidi barani Afrika huku ikikuza ushirikishwaji wa kifedha na maendeleo ya kiuchumi ambayo itasaidia kudhibiti ufisaidi, kuongeza uwazi na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu Tanzania, Profesa Florens Luoga amesema mkutano huo umeshirikisha magavana, manaibu magavana, wakuu wa taasisi za udhibiti na usimamizi wa sekta ya fedha pamoja na watunga sera kutoka taasisi wanachama 32, kutoka nchi 30.

Gavana huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa AfPI, amesema suala la utakatishaji wa fedha limeathiri nchi za Afrika ikiwemo Tanzania na kusababisha zaidi ya Dola za Marekani 350 bilioni hupotea kila mwaka.

Amesema iwapo nchi hizo zingechukua hatua za kudhibiti utakatishaji fedha, upotevu huo ungeweza kushuka hadi Dola 10 bilioni kwa mwaka.

Amesema mkutano huo ambao kwa miaka miwili mfulululizo haujafanyika kutokana na janga la Uviko 19 na kuwa watajadili utoaji wa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao na kuona iwapo zinaleta athari kwa wananchi pamoja na kubadilishana uzoefu wa kupata ufumbuzi wa pamoja wa huduma ya teknolojia.

Kwa upande wa Tanzania, amesema BoT imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wananpata huduma za kifedha umbali usiozidi kilomita 15, lengo likiwa ni kuhakikisha huduma za kifedha zinaweza kubadilisha maisha ya wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa AfPI, Dk Alfred Hannig amesema tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo mwaka 2013 msingi wake ni kusaidia maendeleo ya sera za huduma jumuishi na mipango ya udhibiti.