Miili ya wanandoa waliofariki Mpwapwa yawasili Kilolo

Muktasari:

  • Miili ya Dk Harun Chawala na mkewe Neema Mwasanganga imewasili katika kijiji cha Viwenge wilayani Kilolo mkoani Iringa kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika leo mchana Jumatatu Machi 8, 2021.

Dodoma. Miili ya Dk Harun Chawala na mkewe Neema Mwasanganga imewasili katika kijiji cha Viwenge wilayani Kilolo mkoani Iringa kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika leo mchana Jumatatu Machi 8, 2021.

Wanandoa hao walifariki usiku wa kuamkia Jumapili Machi 7, 2021 baada ya gari lao kutumbukia katika daraja la Shaban Robert lililopo wilayani Mpwapwa.

Dk Chawala alikuwa akimpeleka mkewe aliyekuwa mfanyakazi katika kitengo cha ugonjwa wa kifua kikuu hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.

Kiongozi wa msafara kutoka wilayani Mpwapwa Dk Hamza Mkinguli amesema leo Jumatatu Machi 8 2021 kuwa maandalizi ya makaburi yalikuwa yamekamilika.

“ Tunamshukuru Mungu tumefika salama. Sasa tuko kwenye ibada ya mazishi, tunatarajia ikifika saa 7.00 mchana tutakuwa tunazika,” amesema.

Mbunge wa zamani wa Kilolo,  Venance Mwamoto amesema Dk Chawala alifanya tafiti mbalimbali katika Wilaya ya Kilolo kwa ajili ya kuwasaidia wakazi wa Wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.

“Katika tafiti zake alizozifanya wakati wa uhai wake nyingine alizifanyia Wilaya ya Kilolo na bado alikuwa akiendelea kufanya tafiti ambazo zinaisaidia Wilaya na Taifa kwa ujumla,” amesema.