Mikakati ya Chadema kueleka uchaguzi mkuu 2025

Thursday June 10 2021
mbowepic
By Hamida Shariff

Morogoro. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametaja mikakati ya chama hicho itakayotekelezwa katika kipindi kilichobaki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuifanya Chadema kuwa chama kinachojitegemea kiuchumi na kujisimamia katika utendaji kazi.

Akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Chadema Mkoa wa Morogoro,  Mbowe aliutaja mkakati mwingine kuwa ni kuwatambua na kuwasajili wanachama wao nchi nzima kwa njia ya kidigitali ambayo pia itasaidia kukusanya kikamilifu mapato yanayotokana na michango ya kadi.

Alisema kuwa kupitia usajili wa kidigitali kutasaidia kuwa na idadi kamili ya wanachama.

"Ni bora kuwa na wanachama wachache waaminifu na waliokuwa tayari kukichangia chama kuliko kuwa na wanachama wengi ambao uanachama wao hautambuliki na hawalipii kadi zao na wengine hawana kabisa.”

Katika kukazia hilo Mbowe amesema  Chadema imeazimia kutowaruhusu kuingia kwenye mkutano wanachama wa Chadema wasiokuwa na kadi au ambao kadi zao hazijalipiwa.

Advertisement

Mkakati mwingine ni kujenga ofisi za Chadema wilaya na mikoa yote ya Tanzania ili kukifanya chama hicho kiweze kuwa na ofisi za kisasa zitakazorahisisha utendaji kazi.

Ili kupata viongozi imara na waadilifu ndani ya chama, Mbowe amesema Chadema ina mpango wa kuanzisha taasisi itakayotoa mafunzo ya uongozi kwa wanachama na viongozi watakaotokana na chama hicho.

Kuhusu kuwainua kiuchumi wanachama,  Mbowe amesema Chadema ina mpango wa kuanzisha Saccos itakayokopesha wanachama akisisitiza kuwa ni ujinga kufikiria shida na umasikini ndani ya chama.

Hata hivyo,  yapo mambo ambayo Mbowe ameonesha kutoridhishwa nayo ndani ya Chadema kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi na watendaji wa chama hicho kutowajibika ipasavyo huku wengine wakijikita kwenye shughuli zao binafsi na kuacha ofisi zikiwa zimefungwa na shughuli za chama zikisimama.

"Hatuwezi kufanikiwa kwenye kuongeza wanachama ama kushinda chaguzi kama hatutaweza kuwajibika, muda mwingi ofisi za Chadema kata, wilaya na hata mikoa utazikuta zimefungwa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, niwatake watendaji wa chama kuacha hilo mara moja na mfanye kazi usiku na mchana," amesema Mbowe.

“Kama kuna mtendaji au kiongozi wa chama ambaye anaona amebanwa na shughuli zake binafsi za kazi au biashara na hawezi kufanya shughuli za chama ni heri apishe kwenye nafasi hiyo," amebainisha Mbowe.


Advertisement