Misokoto 5,000 ya Bangi yakamtwa Morogoro

Lilian Lucas

Muktasari:

  • Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslim amesema katika msako walioufanya katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro walifanikiwa kukamata misokoto 5,000 sawa na kilogramu 25 ya bangi.

Morogoro. Polisi mkoani Morogoro inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujihusisha na uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya bangi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 13, 2022, Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslim amesema katika msako walioufanya katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro walifanikiwa kukamata misokoto 5,000 sawa na kilogramu 25 ya bangi.

Amesema tukio la kwanza limetokea katika eneo la kata ya Lukobe ambapo askari wakiwa doria walimkamata Paulo Gaitano (24) mkulima na mkazi wa Mafiga.

Amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa na mkisokoto 5,000 ya bangi akiwa amehifadhi kwenye boksi kwa kuifunika na lailoni nyeusi, huku akiwa ameifunga kwenye pikipiki aina ya Haojue rangi nyeusi.

Tukio la pili kamanda huyo amesema limetokea Mei 22, 2022 eneo la Msamvu Kata ya Mwembesongo ambako alikamatwa Selina Emilia (50) mkazi wa jiji la Dar es Salaam akiwa na bangi viroba viwili sawa na kilogramu 40.

Kamanda huyo alisema mtuhumiwa huyo alikuwa amehifadhi kwenye begi jeusi na kikapu cha rangi ya kijani na nyeusi kiini kikiwa ni kujipatia kipato kinyume na sheria.

Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika