Mjadala cheo, majukumu ya Waziri Mkuchika waendelea

Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalumu), Kapteni Mstaafu George Mkuchika

Muktasari:

Mjadala umeibuka katika mamlaka na mipaka ya kiutendaji kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalumu), Kapteni Mstaafu George Mkuchika ikiwa ni siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza baraza jipya la mawaziri.

Dar es Salaam. Mjadala umeibuka katika mamlaka na mipaka ya kiutendaji kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalumu), Kapteni Mstaafu George Mkuchika ikiwa ni siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza baraza jipya la mawaziri.

Siku nne zilizopita, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa Baraza la Mawaziri lililokuwa na sura mpya na mabadiliko ya wizara, akiwamo Kapteni Mkuchika aliyetumikia Serikali kwa zaidi ya miongo miwili.

Wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 52(1), ikimtambua Waziri Mkuu kuwa na madaraka ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa kazi na shughuli za Serikali, majukumu ya Waziri wa Kazi Maalumu chini ya Ikulu yanategemeana na mahitaji ya Rais anayeweza kumpatia majukumu yeyote.

Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema licha ya Waziri Mkuu kuwa na nguvu kikatiba, hawezi kufuatilia au kuhoji utekelezaji wa majukumu ya waziri mwenye kazi maalumu.

“Mara nyingi nafasi ya wizara hiyo zinahusisha viongozi wazoefu, wenye uwezo mkubwa wa kumshauri Rais, kwa hiyo kazi yake kubwa Mkuchika ni mshauri, hata mawaziri wa ofisi ya Rais wanawajibika kwa Rais kiutendaji haina shida kabisa na imewasaidia sana Zanzibar,” alisema Profesa Bakari.

Wakili wa Kujitegemea, Frank Chacha aliungana na mtazamo huo akisema pamoja na majukumu ya wizara hiyo, bado Waziri Mkuu ana nguvu ya kusimamia utendaji wa shughuli zote za Serikali.

“Waziri Mkuu ndiye msimamizi na anaweza kufuatilia shughuli za wizara hiyo pia. Kazi maalumu haiondoi nguvu kwa Waziri Mkuu, kwa hiyo haina madhara na haivunji sheria,” alisema Chacha akisisitiza hatua hiyo inatokana na mamlaka ya Rais anayeruhusiwa kikatiba kuunda baraza analotaka kwa wakati huo.

“Katika uongozi wake Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki aliwahi kuanzisha wizara ya Nairobi City, ilikuwa ni kazi maalumu, baada ya hapo haikuendelea.”

Wizara hiyo chini ya Kapteni Mkuchika imewahi pia kuongozwa na viongozi mbalimbali wenye uzoefu wa muda mrefu serikalini, akiwamo Profesa Mark Mwandosya alitumikia Serikali ya awamu ya nne.

Hata hivyo, Wakili, Aloyce Komba aliona kuna udhaifu wa kikatiba katika mamlaka ya Rais kutokuwa wazi kwenye uteuzi wa baraza lake la mawaziri, akisema licha ya majukumu mengine kuzingatia masilahi ya Taifa, lakini ilitakiwa katiba kuweka wazi.

“Hilo ni tatizo la kikatiba na hatuwezi kuhoji kwa sababu katiba yetu imetoa mamlaka mengine yasiyojulikana wazi. Katiba ya Marekani imeweka wazi wizara zote zitakazoanzishwa na Rais, sasa naamini suluhisho letu ni mapendekezo ya Katiba mpya yaliyoweka wazi majukumu,” alisema Wakili Komba.