Mjumbe UVCCM ataka siasa za hoja badala ya vioja

Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Victor Makundi akizungumza na vijana wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro. Picha na Florah Temba

Muktasari:

  • Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Victor Makundi amesema Miaka 46 ya CCM iwe kichocheo cha kufanyia kazi changamoto wanazoziona, kuisimamia serikali na kuendesha siasa za hoja badala ya vioja, ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuimarisha chama kupitia vikao, mikutano na kuvutia wanachama wapya kwa sera na siasa safi huku akiwakumbusha vijana kuacha kushinda mitandaoni ovyo.

Rombo. Vijana wa Chama cha Mapinduzi, wametakiwa kujipanga kujibu hoja zinazotolewa na wapinzani kwenye mikutano ya hadhara, ikiwa ni pamoja na kuyasema yale mazuri ambayo yanafanywa na serikali, ili kuwawezesha wananchi kuyafahamu na kuendelea kukiamini chama hicho.

Rai hiyo imetolewa na mjumbe wa baraza kuu la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Victor Makundi wakati akizungumza na vijana wilayani Rombo,  katika maadhimisho ya miaka 46 tangu kuzaliwa kwa CCM.

Makundi amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini, hivyo kama vijana wa CCM, wanapaswa kusimama imara na kujipanga kujibu hoja, na asitokee mtu wa kufanya vioja wala kutoa matusi.

Amesema miaka 46 ya CCM ikawe kichocheo cha kufanyia kazi changamoto wanazoziona, kuisimamia serikali na kuendesha siasa za hoja badala ya vioja, ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuimarisha chama kupitia vikao, mikutano na kuvutia wanachama wapya kwa sera na siasa safi.

“Kuna neno linasema acha mvua inyeshe tuone panapovuja. Ndugu zangu, Rais ameruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya kisiasa, sisi kama vijana wa CCM  tuzidi kusimama imara, tukajibu hoja wala tusifanye vioja na tusitukanane,” amesema Makundi.

Ameongeza kuwa, “Sisi kama vijana wa CCM, tuendelee kuisemea serikali vizuri, yapo mengi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika, na wananchi hawawezi kufahamu  bila sisi kutoka kuwaambia, sasa tukawe mabalozi, tukayaseme yale mazuri yanayofanywa na serikali chini ya CCM.”

Aidha Makundi ametumia pia nafasi hiyo kuwataka vijana kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kuchukua mikopo ya asilimia nne inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya kwa vijana na kuendesha miradi hiyo, ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

“Ndugu zangu vijana, tuchangamkie fursa zilizopo, serikali imetenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri na asilimia 4 ni kwa ajili ya vijana, fedha tumeambiwa zipo, tuache uzembe, tuache kukaa vijiweni, tuache kulalamika na tuache kushinda mitandaoni, sasa tukabuni miradi yetu.”

“Lakini pia niwaase viongozi wa vijana, tuendelee kuupa nguvu umoja wetu, tutunze amani ya nchi, tushirikiane na tuchape kazi kwa bidii”.

Akizungumza mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Rombo, Evance Mrema amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kukemea maovu katika jamii, ikiwemo vitendo vya kikatili, wizi, uporaji na ulevi wa kupindukia.

“Katika maadhimisho haya ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM, vijana tunakumbushwa kuwa wazalendo na kutambua tunalo jukumu la kuilinda dola ili iendelee kubaki mikononi mwa CCM”

“Lakini pia kama vijana, tunapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea maovu katika jamii, ikiwemo matukio haya ya unyanyasaji na ukatili ambayo yametajwa kuongezeka, pamoja na ulevi wa kupindukia katika jamii”.

Viongozi hao pamoja na viongozi wengine wa UVCCM Wilaya ya Rombo, pia walitembelea shule ya sekondari Mamsera pamoja na Kelamfua, ambapo pamoja na kupanda miti, walizungumza na uongozi wa shule pamoja na wanafunzi, ili kubaini changamoto zilizopo na kuzisemea serikalini, ili ziweze kupatiwa ufumbuzi