Mkakati wa NBS kwa sensa mpya

  • Kaimu Meneja wa Shughuli za Kitakwimu Benedict Mugambi (mwenye mavazi ya bluu)  akizungumza na Wananchi na Viongozi wa Kata ya Makuru jijini Dodoma wakati wa zoezi la majaribio la Kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ngazi ya Vitongoji.

Muktasari:

  • Kwa mara ya mwisho sensa ya watu na makazi ilifanyika mwaka 2012, ambapo mwakani Watanzania wataingia tena kwenye zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Dodoma. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imepanga kutumia vitongoji au mitaa wakati wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani ili kupunguza gharama na kutumia muda mfupi kuikamilisha.

Akizungumza wakati wa majaribio ya kutenga maeneo kwa kutumia vitongoji, Kaimu Meneja wa Shughuli za Kitakwimu wa NBS, Benedict Mugambi amesema kutokana na muda uliobaki, wameamua kutumia vitongoji kutenga maeneo ya kuhesabia watu.

“Leo tupo hapa Kata ya Makuru wilayani Manyoni, Singida kufanya majaribio ya kutenga maeneo kwa kutumia vitongoji. Tumebakiwa na muda mfupi sana kufikia sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022,” amesema Mugambi.

Mugambi amesema hadi kufikia Mei, mwaka huu, mikoa ambayo zoezi la kutenga maeneo limekamilika ni pamoja na Dodoma na Singida huku kazi hiyo ikiendelea mkoani Manyara ambako imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Naye Ofisa Mipango Miji kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, George Milingai amesema kazi hiyo inafanyika kwa ushirikiano kwa kuwa, Tamisemi ni mdau mkubwa wa matumizi ya taarifa hizo za sensa.

Naye Diwani wa Kata ya Makuru, Moses Matonya amesema sensa ni jambo muhimu kwa maendeleo hivyo, watahakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali ili kufanikisha zoezi hilo kwa wakati.

Matonya amesema watahamasisha wananchi waendelee kushirikiana na Serikali ikiwemo ikiwemo kuibua changamoto na fursa mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao.

Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine itafanya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022. Sensa hii inafanyika ikiwa imepita miaka 10 toka kufanyika ya mwisho mwaka 2012.