Mkakati wa Rais Samia

Mahojiano maalumu na Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza mwaka mmoja tangu achukue madaraka ya nchi, pamoja na maendeleo aliyoyasimamia amebainisha mikakati yake muhimu katika kuijenga nchi.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza mwaka mmoja tangu achukue madaraka ya nchi, pamoja na maendeleo aliyoyasimamia amebainisha mikakati yake muhimu katika kuijenga nchi.

Mbali na hayo, alisema amedhamiria kuleta mabadiliko kwenye Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kufanya mabadiliko kidogo kwenye Jeshi la Polisi, kufanya mapinduzi kwenye kilimo cha umwagiliaji, Tanzania anayoitaka.

Hata hivyo, amesema ‘anachokimisi’ kwenye nafasi ya urais ni uhuru.

Rais Samia aliyasema hayo kwenye mahojiano maalumu ya kutimiza mwaka mmoja tangu aapishwe kushika madaraka ya nchi Machi 19, 2021, yaliyofanyika Jumapili ya Machi 13, 2022 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye mahojiano hayo yaliyoongozwa na Bakari Machumu, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd - wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na Mwananchi Digital, Rais vilevile aliyataja mambo yaliyompa matumaini katika kuiongoza nchi kuwa ni uzoefu wake serikalini, ndani ya CCM na uwezo wa kujieleza kwa Watanzania.

Alipoulizwa swali namna gani anafanya maamuzi magumu, Rais Samia alisema, “ni kutaka ushauri, nashauriana na wenzangu sifanyi mwenyewe, nashauriana na wenzangu, mshauri wa kwanza, wa pili, wa tatu naangalia, napima nafikia pa kufanya maamuzi.

“Kila kitu ni ushauri. Hakuna mwanadamu anaweza kufanya kila kitu mwenyewe na ndiyo maana tumewekewa wasaidizi. Kwa hiyo ni ushauri na wenzangu,” alifafanua.

Kuhusu kitu gani anakikosa kwa kushika wadhifa mkubwa wa mamlaka ya juu katika nchi, alisema: “Uhuru, uhuru wangu tu, nakabwa kila pembe, huwezi kuzunguka, kutembea. Zamani nilikuwa naweza kusimama hapa naita wee Zuhura weeee, weee nini, wewe njoo. Sasa sithubutu.”

Hata hivyo, alisema anachokifurahia ni kulihudumia Taifa lake na atafanya kwa hivyo kadiri Mungu alivyomjaalia.

“Kwa hiyo nikiona mambo mazuri yanatokea basi yananipa faraja,” aliongeza.

Pia, Rais Samia alitumia fursa hiyo kuelezea Tanzania anayotaka kuiona -- ya Watanzania wasiokubali kuchochewa kuharibu utaifa wao, inayodumisha amani na utulivu.

Alisema anataka kila Mtanzania aweze kupata mahitaji muhimu, ikiwemo chakula kila siku.


Uwekezaji TTCL

Rais Samia amesema Serikali yake haitasita kuingia ubia na shirika kubwa la ndege kwa lengo la kuifanya ATCL iweze kufanya biashara kwa faida.

Katika kuliboresha shirika hilo, alisema wataangalia operesheni zake kama ni abiria, ni mizigo, wapi kuna mizigo mingi, wapi kuna abiria wengi na njia zipangwe vipi.

Rais Samia alisema katika kufanya hivyo hawatasita hata kuingia ubia na shirika lingine lenye nguvu zaidi katika kufanya kazi hiyo.

Serikali katika awamu ya tatu iliwahi kuingia ubia na Shirika la Ndege la Afrika Kusini, lakini baadaye ushirikiano huo ulisitishwa baada ya kuonekana haukuwa na tija.

Swali: Mheshimiwa Rais, katika uwekezaji kwenye shirika letu la ndege, ningependa kujua Serikali yako ina mpango gani kuweka mazingira yatakayoiwezesha ATCL ijiendeshe kifaida?

Jibu: Unajua shirika la ndege lina mambo mengi. Shirika la ndege kwa ndani kwanza ni viwanja ambavyo tunaendelea na ujenzi wa viwanja, tuko Songea, Mwanza tunafanya ukarabati tunaongeza uwanja, lakini tuko Chato, uwanja tunaendelea kujenga, juzi juzi hapa nilipotoka Brussels (Ubelgiji) nilikwenda kukwamua mradi wa kiwanja cha ndege cha Kigoma, Pemba, Tanga na viwanja vingine vinaendelea kujengwa, Iringa pale Nduli kinaendelea kujengwa.

Kwa hiyo kwanza, ni viwanja, lakini tusisahau Msalato hapa Dodoma ambao wakandarasi wako kwenye site pale wameanza. Kwa hiyo kwanza ni viwanja, lakini pili, ni ununuzi wa ndege ambapo kama mnavyojua 11 ziko tayari, tano tunasubiria kuzipokea na tutaendelea kununua kuongeza stock ya ndege jinsi tunavyokwenda.

Tatu, ni menejimenti na operesheni ya shirika lenyewe, kwa hiyo kwenye menejiment na operesheni tunakusudia kulisoma shirika letu la ndege, kulifanyia rating (kulipima), kwa nini halifanyi kwa faida, limerithi madeni makubwa, tunatoaje yale madeni makubwa ambayo yamerithiwa kwenye vitabu vya shirika.

Kwa sababu madeni yale unapotia thamani ya shirika madeni yanakuja juu, shirika linakuwa muda wote halifanyi faida, kwa hiyo kwanza ni kufuta hayo madeni ya nyuma, tukubaliane kama Serikali tunafanyaje kitaalamu kufuta madeni ya nyuma. Lakini ili liongeze ufanisi menejimenti ikoje, wafanyakazi wakoje, contribution (mchango) ya wafanyakazi kwenye shirika ikoje. Kuna factors (vigezo) nyingi tutakwenda kuzitazama kwenye hiyo.

Lakini, pia kwenye operesheni zake, je, ni abiria, ni mizigo, wapi kuna mizigo mingi, wapi kuna abiria wengi, route (njia) zipangwe vipi. Na katika kufanya hivyo hatutasita hata kuingia ubia na shirika jingine ambalo lina nguvu zaidi tukafanya kazi kwa pamoja.

Kama tunaingia ubia kwenye madini, kwenye mashimo yetu ya mali na hapa tunaweza tukaingia ubia wakatusaidia kwenye operesheni na menejimenti ya shirika lenyewe, uendeshaji na uongozi wa shirika lenyewe.

Kwa hiyo kwenye shirika la ndege ni kweli kuna changamoto zake, tutakaa tuzitazame, tunajipanga kwenye hilo.

Swali: Kuna mawazo yaliwahi kutolewa kwamba pengine katika nchi za Afrika Mashariki nchi nne zina mashirika ya ndege. Je, fikra zinaweza kuturudisha nyuma kuwe na shirika moja la ndege.

Jibu: Likianzishwa kwenye jumuiya tutalijadili.

Swali: Maelezo uliyoyatoa kuhusiana na usafiri wa anga linahusiana na suala la utalii. Utalii wa Tanzania umekuwa ni kuangalia wale watalii wenye uwezo mkubwa. Je, mwelekeo wetu utaendelea kuwa huo au kutakuwa na mabadiliko kidogo?

Jibu: Labda kidogo nisemee mwelekeo. Tanzania tulianza na watalii wa hali ya chini. Ndio tulianza nao. Kwa Zanzibar kule, kwa mfano, tulianza na Wataliano na tulikuwa tunapokea wale wafanyakazi wa Serikali na wale ambao wameshalipa wanakotoka, lakini tukabadilika kwa kuongeza huduma na hadhi ya mahoteli, tukatoka kwenye two stars, three stars (nyota mbili, nyota tatu) hizo tukapanda mpaka tukafika kwenye nne maeneo mengine, maeneo mengine tuna tano.

Sasa jinsi unavyopandisha viwango vya mahoteli ndivyo unavyopata watalii wakubwa. Lakini watalii wakubwa kwenye nchi huwezi kwenda na watalii wakubwa peke yao, kwa sababu kuna mahoteli haya ya chini huku na yenyewe yanahitaji watalii.

Kwa hiyo nadhani tunakwenda na wote, wakati tunatilia mkazo kujenga mahoteli mazuri, makubwa ili yalete wenye pesa wanaotumia sana, lakini hata wale wengine wataendelea kuja kwa sababu kuna watakaokuja kwa mafunzo kujifunza na kuna watakaokuja kwa utafiti na kutembea, hatuwezi kuwaepuka.

Kwa hiyo mwelekeo wetu tunakwenda na wote tunapandisha hadhi yetu kwenye utalii, lakini na hawa nao tunakwenda nao.

Swali: Hivi Watanzania kujitokeza na kuwa na hamu ya kwenda kwenye vivutio vilivyopo nchini, msukumo wa domestic tourism (utalii wa ndani) ukoje.

Jibu: Tunalipa msukumo mkubwa, kwa sababu mimi nililishuhudia Desemba, nilikwenda Ngorongoro na nilikuta idadi kubwa sana wenyeji wako kule na watoto.

Kwa hiyo unaona kabisa ukiweka mazingira mazuri watu wa ndani wanakwenda wanatalii kwenye maeneo, tutaendelea nalo ili watoto wetu si tu kwenda kutembea, lakini wanajifunza.

Mimi nilikwenda na wajukuu na wamejifunza mengi, nikawapeleka mpaka kule kwenye makumbusho, wameuliza maswali mengi mpaka unashangaa hawa wanaweza kuuliza maswali haya. Kwa hiyo watoto wakipelekwa wanajifunza na wanakua wakiwa wanaijua nchi yao vizuri. Kwa hiyo tutalipa msukumo mkubwa tu.

Maswali kibao kichwani

Swali: Mheshimwa Rais ukipiga picha mwaka mmoja nyuma, ukiangazia saa 72 tangu ulipopewa taarifa ya kifo cha Rais wa awamu ya tano John Magufuli na saa 72 baadaye unakwenda kuapishwa kuchukua majukumu ya kuongoza nchi yetu. Unaweza kutupitisha katika kipindi kile cha mabadiliko makubwa na mshtuko, lakini sasa kuelekea kwenye kuchukua usukani wa kuongoza nchi yetu nini kilikuwa kikitembea kichwani mwakao?

Jibu: Kwanza mshtuko kama ulivyosema. Huzuni ya kuondokewa na kiongozi wetu, Rais aliyekuwa madarakani, lilikuwa ni jambo kubwa sana. Tanzania hatujawahi kuona hiyo, tunaondokewa na marais lakini baada ya kustaafu. Aliye madarakani ilikuwa ni mara ya kwanza na bila shaka ilileta hofu, si kwangu tu, lakini kwa Watanzania wengi, (tulijiuliza) sasa itakuwaje. Baada ya hofu kinachofuata nikijua Katiba inasema nini kwenye nchi yetu linapotokea tukio hili, nilijawa na woga na wasiwasi, itakuwaje, nitawezaje, nikiona yale tuliyoyafanya kwenye awamu ya tano najiuliza mimi nitayawezaje, nitayaendelezaje?

Kwa hiyo ulikuwa wakati mgumu kama ulivyosema na pengine hauelezeki. Sijui, hauelezeki lakini ulikuwa wakati mgumu. Kwa hiyo, mpaka ninaapa kama nilivyosema wakati ule mwanzo, nimeapa kwa woga mwingi sana.

Tumezoea ukimaliza kuapa unasikia vigelegele vya kina mama, wanaume wanapiga makofi. Siku ile haikuwa hivyo, akili yangu ilikuwa inaniambia nimetwika mzigo wakati mgumu, sijui itakuwaje.

Mwenzetu aliyetutoka hatujamsitiri, nitawezaje, mambo mengi yalikuwa yanakuja kichwani, lakini kwenye ushirikiano, kwenye miongozo, kwenye mfumo uliwekewa misingi, basi mambo yanakwenda kama misingi inavyoongoza. Hatimaye tumeweza kuvuka salama na tumefika tulipofika leo.

Swali: Nini kilichokuwa kinakupa matumaini, umepita kwenye kipindi hicho, sasa umebaki peke yako. Nini kinakupa matumaini?

Jibu: Matumaini ni kwamba kwanza nilijua kilichotokea ni kazi ya Mungu na kama ni kazi ya Mungu, Mungu huyohuyo ndiye atanisimamia na vitabu vinasema mamlaka hutoka kwa Mungu. Sasa kama Mungu aliniteua mimi nikae hapo kwenye mamlaka, nilijua Mungu atanipa uwezo nitaweza.

Lakini la pili kilichonipa matumaini ni kwamba mfumo wetu Tanzania una maelekezo ya kikatiba ya mipango ya maendeleo ya nchi ya dira zetu ya ilani, mambo yote yamesha elekezwa, kwa hiyo kinachokuja kwako ni kutumia vizuri vyombo vyako, watu wako, uhusiano wako ili uweze kuyakamilisha yale ambayo yameelekezwa.

Lakini, la tatu nilijua Tanzania Mungu ametubariki na roho rahim. Watanzania ukiwaeleza jambo wakilielewa na wakilikubali mambo yanakwenda vizuri. Kwa hiyo nilijua kama nitajieleza vizuri kwa Watanzania watanikubali, watanipa ushirikiano tutakwenda vizuri na ndicho kilichotokea.

Kwa hiyo mambo matatu hayo makubwa, ndiyo yamenipa msukumo mkubwa.

Lakini pia la nne labda uzoefu, uzoefu katika mambo ya Serikali, kwa sababu nimeshakaa serikalini kwa miaka mingi, nikianza na ngazi za chini, nimeingia serikalini mwaka 1977, kwa hiyo mpaka yale yanatokea mwaka 2021 ni miaka mingi kidogo. Na nimekwenda ngazi kwa ngazi mpaka kufika huko, kwa hiyo nilijua nina uzoefu mkubwa ndani ya Serikali, lakini pia ndani ya chama chenye ilani inayotakiwa kutekelezwa nina uzoefu mkubwa pia.

Kwa hiyo pia ilinipa matumaini kwamba nitaweza.

Swali: Sekta ya habari bado kuna changamoto kubwa. Je, Serikali itafanya nini kuhakikisha kwamba ustawi na uwekezaji zaidi unatokea katika sekta hii unganishi kwa maendeleo ya jamii.

Jibu: Umesema bado kuna changamoto kubwa, ningeijua hiyo changamoto ningekupa jawabu la changamoto.

Swali: Ni suala la uwekezaji kwa maana kujiendesha kiuchumi. Mfano kwa sasa bei za karatasi zimepanda sana zaidi ya mara mbili ndani ya miaka miwili.

Jibu: Suala lako ni zuri, lakini ukiangalia pia suala la ufanyaji biashara na ushindani na mabadiliko ya uchumi wa dunia tunakokwenda.

Karatasi imepanda bei, kila kitu kimepanda bei. Uviko-19 sababu moja, vita ya Urusi na Ukraine sababu ya pili inapandisha sana bei ya mafuta na kwa maana hiyo kila kitu kitapanda bei.