Mke wa Bilionea Msuya kujitetea mwakani

Mke wa Bilionea Msuya kujitetea mwakani

Muktasari:

  • Mke wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini marehemu Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita anatarajia kujitetea Machi mwakani katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.

Dar es Salaam. Upande wa mashitaka katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili mke wa aliyekuwa mfanyabiashara wa madini, marehemu Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mfanyabiashara Revocatus Muyella wamefunga ushahidi baada ya shahidi wa tatu kukamilisha kutoa ushahidi wake.

Kesi hiyo ndogo inatokana na mshtakiwa wa kwanza Miriam Mrita, kupitia Wakili wake Omary Msemo kupinga maelezo yake ya onyo yasipokelewe mahakamani kama ushahidi na kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuteswa wakati wa kuchukuliwa maelezo hayo.

Akitoa ushahidi wake, shahidi watatu katika kesi hiyo Deogratius Kallanga (36) ambaye ni daktari wa binadamu katika hospitali ya Temeke alidai Januari 2017 akiwa katika kituo chake cha kazi alimfanhyia vipimo mshtakiwa wa kwanza.

Akiongozwa na wakili wa Serikali Caroline Matemu mbele ya Jaji Edwin Kakolaki, Kallanga ambaye ni Mkuu wa idara ya magonjwa ya dharura alidai Januari 18, 2017 akiwa kituo chake cha kazi aliwapokea watu wawili walipelekwa na askari ambapo alikuwepo mwanaume na mwanamke.

"Baada ya kufika mwanamke alidai ana maumivu kwenye nyonga ya mguu wake wa kushoto na katika bega la kulia baada ya kumuangalia nikaona ana tatizo kwenye misuli, lakini kwa kuwa alikuwa na askari nikaona nimpime ili kujiridhisha kama amepigwa," amedai shahidi huyo.

Amedai baada ya vipimo vilionyesha yuko sawa na kumuandikia dawa, kwani hakuwa na tatizo kubwa na kwa utaalamu wake yalikuwa ni maumivu ya kawaida ya misuli.

"Baada ya kumuhudumia nilijaza fomu ya matibabu kutoka polisi (PF3) kutokana na uchunguzi huo alikuwa akilalamika kuwa alipigwa na polisi miezi kadhaa iliyopita hivyo kuamua kumfanyia vipimo vilivyooknyesha alikuwa na maumivu ya kawaida ya misuli," amedai Shahidi huyo.

Hata hivyo, baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi, Wakili wa Serikali Gloria Mwenda alisema kwa upande wao wamefunga ushahidi kwa kuita mashahidi watatu.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Omary Msemo wamedai kuwa katika utetezi wao watakuwa na mashahidi watatu akiwemo mshtakiwa mwenyewe na kuiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa mteja wake hajisikii vizuri.

Jaji Kakolaki amesema kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa siku tatu mfululizo, hivyo kutokana na kalenda ya mahakama kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Machi 2022 ambapo mshtakiwa wa kwanza katika kesi ndogo ataanza kujitetea.