Mke wa Sabaya atoa ushahidi

Muktasari:
- Mke wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Jesca Thomas (28) ameieleza Mahakama namna walivyokamatwa na mume wake na askari waliokuwa na silaha jijini Dar es Salaam.
Arusha. Mke wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Jesca Thomas (28) ameieleza Mahakama namna walivyokamatwa na mume wake na askari waliokuwa na silaha jijini Dar es Salaam.
Jesca ambaye ni shahidi wa pili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Sabaya na wenzake sita ameieleza Mahakama kuwa alikamatwa na mume wake Mei 27 mwaka jana jijini Dar es Salaam ambapo alidai kabla ya kukamatwa walipekuliwa na askari hao waliokuwa wamevalia kiraia huku wakiwa na silaha.
Leo Januari 17, 2022 akiongozwa na Wakili Mosses Mahuna anayemtetea Sabaya, Jesca alijitambulisha mahakamani hapo kuwa ni mke wa mshitakiwa huyo na walifunga ndoa mwaka 2018.
"Tukiwa chumbani walikuja watu usiku, walikuwa wanagonga kwa nguvu sana na hawakusubiri kufunguliwa walitumia njia zao wakaingia ndani ilikuwa ni saa 10 jioni. Walivyoingia Lengai akauliza ni nini na ni nani nyie, wakajibu wakasema ni askari wakatuamuru tukae sehemu moja,"
"Wengine wakawa wanapekua kabati mabegi wakatoa na godoro wakapekua kila mahali, vurugu kila kitu kikavurumushwa kule ndani,walivyomaliza wakasema tunaondona na nyie tunaenda Takukuru,na hawakutufahamisha chochote kabla ya kutupekua," amedai
Shahidi huyo amedai mahakamani hapo kuwa walikamatwa wao wawili na baada ya kutoka makao makuu ya Takukuru, Upanga walisafirishwa Juni 3 usiku na kufikishwa Arusha ambapo pamoja na vitu vingine walikabidhi gari aina ya Land Cruiser V8, lenye namba za usajili T 222 BDY ambayo walikutwa nayo, pesa pamoja na simu.
Amedai gari hilo Sabaya alinunua Oktoba 2020 kutoka kampuni ya Oil Com na ambaye alisimamia mauziano hayo alimtaja kwa jina la Said.
Kuhusu namba ya simu 0758 707171 inayodaiwa kuwa ya Sabaya, Jesca ameieleza mahakama kuwa namba hiyo imesajiliwa kwa jina la mume wake na wamekuwa wakiitumia wote ambapo yeye anaitumia kwa ajili ya kufanya biashara.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga shahidi huyo alidai kuwa wana magari mawili ambayo yote ni Land Cruiser VX V8 yote yanashikiliwa Takukuru
Sehemu ya mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo;
Wakili: Nikumbushe majina yako
Shahidi: Jesca Thomas Nassari
Wakili: Wewe na Lengai Sabaya hamjawahi kufunga ndoa
Shahidi:Tumefunga ndoa
Wakili: Mlifunga ndoa lini?
Shahidi: Sabato Central Church mwaka 2018
Wakili: Cheti cha ndoa cha hilo kanisa unacho?
Shahidi:ndiyo
Wakili:Kipo nyumbani mna mpango gani?
Shahidi:Kikihitajika nitakileta
Wakili:Leo ulijua unatoa ushahidi mbona hukukileta?
Shahidui:Sikuwa nakuja kuthibitisha ndoa ndiyo mana sikukileta
Wakili:Umekuja kufanya nini?
Shahidi:Kutoa ushahidi wa kesi inayoendelea mahakamani lakini si ya ndoa
Wakili:Tutajie wasimamizi wa ndoa yenu
Shahidi:Ni Elibariki Nnko na Ruth Urassa
Wakili:Wako hapa Arusha
Shahidi:Wanakaa Dar Es Salaam
Wakili:Umesema unafanya biashara gani?
Shahidi:Nauza na kununua maharage na mahindi
Wakili:Unauza kibaba debe au gunia?
Shahidi:Inategemea mteja anahitaji kiasi gani
Wakili:Una warehouse ya kuhifadhi mazao ghala liko wapi?
Shahidi :Kisongo na lingine liko Tengeru
Wakili:Umekodi kwa nani?
Shahidi:mzee Metili
Wakili:Kiasi kikubwa cha mahindi na maharage ulichowahi kuuza?
Shahidi:Gunia 200,300 sijawahi kuzidisha
Wakili:Haumiliki kampuni
Shahidi:Ni kweli
Wakili:Hauna hata leseni
Shahidi:Biashara ninayofanya mimi haihitaji leseni
Wakili:Kwa hiyo hauna
Shahidi:Eeh
Wakili:Kwa hiyo haulipi kodi
Shahidi:Ninalipa ushuru
Wakili:Wapi
Shahidi:Sokoni
Wakili:Hauwezi kulipa ushuru sokoni wa gunia 200
Shahidi:Siwezi kuuza zote kwa pamoja
Wakili:iyo biashara ni ya kwako personal?
Shahidi:Tulikuwa tunafanya pamoja na Sabaya ila mimi ni msimamizi
Wakili:Kwa hiyo na Sabaya alikuwa anafanya biashara bila leseni?
Shahidi:Nimeshasema kwa aina ya biashara na mfumo tunaotumia hauhitaji kuwa na leseni
Wakili:Hizo biashara zenu za mahindi na maharage mmeanza mwaka gani
Shahidi:2018
Wakili:Mmeshatengeneza kiasi gani?
Shahidi:Siwezi kujua kwa sababu ni fedha ambayo iko kwenye mzunguko
Wakili:Kwa biashara hii ambayo mimi naiona ni ndogo sana mtaji wenu ulikuwa kiasi gani?
Shahidi:Siwezi kujua manake fedha ziko kwenye mzunguko
Wakili:Wakati mlipoanza 2018
Shahidi:Milioni tatu
Wakili:Jesca unakubaliana na mimi biashara yenu ni ndogo sana labda uniambie mtaji wenu?
Shahidi:Nimesema fedha ziko kwenye mzunguko
Wakili:Umeshawahi kufanya assesment ya biashara?
Shahidi:Sikumbuki
Wakili:Umesema umekaa na Sabaya na miaka minne?
Shahidi:Mitano sasa inakuwa
Wakili:Mitano mingi,Sabaya hana kampuni
Shahidi:Ni kweli
Wakili:Hakuna biashara nyingine wewe na Sabaya zaidi ya mahindi na maharage?
Shahidi:Tunafanya ufugaji ambapo kwenye kufuga tunauza pia
Wakili:Ulisema mnafuga nini
Shahidi:Ng'ombe, kuku na mbuzi
Wakili:Wewe na Sabaya mna kuku wangapi?
Shahidi:Mara ya mwisho niliwahesabu wako 600
Wakili:Wako wapi?
Shahidi:Wako Malula
Wakili:Mna ngonbe wangapi?
Shahidi:Mimi sijawahi kuwahesabu Lengai ndiyo anawahesabu
Wakili:Wewe ni mke wa Sabaya na haujui ngombe wake
Shahidi:Yeye ndiyo anapenda kuhesabu
Wakili:Umewahi kuuza ngombe lini?
Shahidi:Mdiyo mwaka jana mwezi wa nane
Wakili:Mwaka jana umeuza wa ngapi?
Shahidi:Lengai ndiyo anajua
Wakili:Wewe ni mke ng'ombe zinauzwa haujui idadi?
Shahidi:Nataka kujua kilichopatikana
Wakili:Mwaka juzi 2020 Sabaya aliuza ngombe wangapi
Shahidi:Sijui
Wakili:Haujawahi kujui Sabaya ameuza ngombe wangapi mwaka 2020?
Shahidi:Sifahamu
Wakili:2019
Shahidi:Sifahamu
Wakili: 2018
Shahidi:Sifahamu
Wakili:Umesema hautaki kujua idadi unataka kujua kiasi mwaka jana alipata kiasi gani?
Shahidi:Mwaka jana hapana hakuuza
Wakili:Mwaka 2020 alipata kiasi gani kwa kuuza ng'ombe?
Shahidi:Kwa hela aliyokuja nayo 2020 ilikuwa Milioni 20
Wakili:Katika mauzo hayo ingawa wewe ulikuwa hauzingatii idadi ya mifugo mlikuwa mnalipa kodi?
Shahidi:Tulikuwa tunalipa ushuru mnadani
Wakili:Sabaya alikuwa ana chanzo kingine cha mapato?
Shahidi:Mshahara
W mbuzi anao wangapi
S sijawahi kuhesabu
Wakili:Nani anachunga mbuzi na ngombe huko shamba?
Shahidi:Kuna watu wako huko shamba
Wakili:Shamba la nani?
Shahidi:La kwetu
Wakili:La wewe na Sabaya
Shahidi:Ndiyo
Wakili:Shamba la heka ngapi Jesca?
Shahidi:11
Wakili:Umesema wewe na Sabaya mnamiliki magari mangapi?
Shahidi:Mawili namba T 341 ANT na T 222 BDY
Wakili:Gari la tatu
Shahidi:Ni hayo tu ninayoyafahamu
Wakili:Hiyo T 341 ATN ilinunuliwa ukiwa kwenye ndoa?
Shahidi:Ndiyo
Wakili:Na hii T 222 BDY ilinunuliwa ukiwa kwenye ndoa?
Shahidi:Ndiyo
Wakili:T 222 BDY mliinunua kwa Sh.milioni 60?
Shahidi:Hapana, tuliinunua kwa kuvunja unatoa gari unajazia hela kidogo unachukua gari
Wakili:Na wewe Sabaya unampenda sana ndiyo mana unahudhuria kesi yake?
Shahidi:Kwa ajili ya kujua mwendelezo wa kesi si kumpenda
Wakili:Ndiyo mana nakuona hapa tena
Shahidi:Kujua mwendelezo wa kesi
Wakili:Shahidi wa 12 ulimsikia hapa mahakamani si ulikuwepo na ulimsikia
Shahidi:Ndiyo
Wakili:Pole lakini mume wako anashitakiwa umekuwa mwaminifu kuwasikikiza mashahidi wote
Shahidi:Ndiyo
Wakili:Shahidi Sabri alisema gari T 222 BDY walimuuzia Sabaya na ulitolewa mkataba wa mauziano wa lile gari kama kielelezo
Shahidi:Ndiyo
Wakili:Ule ndiyo mkataba wenyewe?
Shahidi:Mkataba wenyewe nimeutoa mimi na si ule
Wakili:Kadi ya gari namba T 222 BDY inasomeka jina la Sabaya na si la kwako
Shahidi:Ndiyo
Wakili:Na hilo lingine?
Shahidi: Linasomeka jina la kwangu
Wakili: Alikununulia Sabaya
Shahidi: Tulinunua pamoja
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Januari 18, shahidi huyo atakapoendelea kuhojiwa na mawakili wengine wa Serikali.