Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro apiga marufuku wananchi kuvamia msitu
Muktasari:
- Msitu wa asilia wa Chome uliopo katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro upo hatarini kutoweka kutokana na uvamizi wa mipaka, ukataji wa miti pamoja na uchomaji wa moto kiholela hali ambayo inatishia kukauka kwa vyanzo vya maji katika msitu huo.
Same. Uoto asilia wa Msitu wa Chome, uliopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro upo hatarini kutoweka kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu hali ambayo imesababisha baadhi ya vyanzo vya maji kukauka na kutishia hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu leo Januari 27, 2023 amepiga marufuku wananchi wanaozunguka hifadhi ya msitu huo kuingia kinyemela na kufanya shughuli za kibinadamu ili kuunusuru msitu huo ambao ni wa aina yake.
Babu amepiga marufuku hayo leo, Januari 27 wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo la msitu huo na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na wadau wa Tawi la Mashariki (EAMCEF) za kuunusuru msitu huo.
Hata hivyo, Babu amewaagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika wilaya hiyo kuhakikisha wanashirikiana na wananchi wanaozunguka hifadhi ya msitu huo na kuzungumza lugha moja ili waweze kuulinda msitu huo ambao uko hatarini kutoweka.
"Hii misitu inatakiwa ihifadhiwe, hii misitu ndio uhai, ikihifadhiwa vizuri inasaidia vyanzo vyetu vya maji ambavyo vinasaidia wananchi wetu walio maeneo ya chini kupata maji. Sasa huku juu kuna tatizo ambalo lipo la watu kuchoma misitu ovyo na kwa makusudi kwa mambo wanayojua wao," amesema.
"Watu wanakata miti bila mpangilio na nimeambiwa watu wanakata miti kwa wizi kwa ajili ya shughuli zao kwa kujipatia kipato bila kuzingatia utaratibu, sasa kwa jambo la uhifadhi lazima TFS mhakikishe ninyi pamoja na vijiji vinavyowazunguka mnazungumza lugha moja," amesema.
Aidha Babu amepiga marufuku wananchi wa mkoa huo, kukata miti waliyoipanda bila kuwa na kibali.
"Hakuna kukata miti bila kibali, hata kama mti ni wa kwako lazima hatua zote zifanyike kuanzia ngazi ya kijiji na hata ukikata mti mmoja lazima upande miti kadhaa," amesema.
Naye, Kamanda Msaidizi TFS Kanda ya Kaskazini, Yusufu Kajia amesema msitu huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ya uvamizi wa mipaka, uchimbaji wa madini, matukio ya uchomaji wa moto, uvunaji haramu wa miti ya mbao na mazao ya misitu yasiyo ya mbao.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo ulianzishwa Mfuko wa Hifadhi ya milima ya Tawi la Mashariki (EAMCEF) ili kupunguza uharibifu katika msitu huo, kuongeza uoto wa asili, kuimarisha na kuongeza utalii katika hifadhi hiyo na kuinua ustawi wa jamii kuzunguka hifadhi ya msitu huo.
Emannuel Kiengi ambaye ni afisa maliasili mkoani humo, amesema mradi wa EAMCEF umelenga pia kuisaidia serikali katika juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira ya msitu wa chome pamoja na mambo mengine.
"Kupitia mradi huu tumeweza kuibua vikundi mbalimbali vya vijana ikiwemo kufanya shughuli za ulinzi shirikishi katika maeneo haya ili kuhakikisha wanapambana na wale wote wanaofanya shughuli za uharibifu wa mazingira," amesema.