Mkuu wa wilaya asisitiza matibabu bure kwa watoto, wazee

Mkuu wa wilaya asisitiza matibabu bure kwa watoto, wazee

Muktasari:

  • Hatua hiyo imetokana na malalamiko ya wananchi kwamba, wamekuwa wakitozwa Sh4000 kama gharama za huduma za afya kwa ajili ya watoto.


Njombe. Serikali imeonya tabia ya uongozi wa Kituo cha Afya Makambako, kuacha mara moja kuwatoza fedha za matibabu watoto chini ya miaka mitano.

Imesema kuwa kuwatoza fedha kwa ajili ya matibabu ni kinyume na Sera ya Afya ambayo inawataka kupatiwa matibabu bure.

Onyo hilo limetolewa leo Mei 13, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri kufuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi kwamba, wamekuwa wakitozwa Sh4000 kwa ajili ya matibabu ya watoto chini ya miaka mitano.

Ruth amesema kuwa Sera ya Afya inataka mtoto chini ya miaka mitano kutibiwa bure hivyo, wanapaswa uongozi wa kituo hicho hawana budi kutekeleza.

“Kinachofanyika huko Makambako sikiungi mkono hata kidogo, walishawahi kuniambia kuwa wamefuta hivyo wasirudie tena,” amesema Ruth.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Hanana Mfikwa amekiri kuwepo kwa tatizo hilo hapo awali kutokana na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu Sera ya Afya.

Hata hivyo, amesema kuwa kwa sasa wamefuta utaratibu wa kulipia huku watoto chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wasiojiweza wanapatiwa matibiwa bure.

“Nikiri kuwa tatizo hili la watoto kutozwa fedha lilikuwepo baada ya kulifuatilia na tumeweka utaratibu kuwa watoto, wajawazito na wazee hawataendelea kutozwa. Kwa sasa watoto wote chini ya miaka mitano wanapata huduma bure. Jambo la msingi ni wazazi kwenda na kadi,” amesema  Mfikwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Paul Malala amewataka wananchi kuzitumia zahanati zilizojengwa kwenye kata mbalimbali kupata huduma badala ya kutembea umbali mrefu kwenda Kituo cha Afya Makambako.

Baadhi ya wananchi mjini Makambako wameishukuru Serikali kwa kurejesha utaratibu wa matibabu bure kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa kuwa imewapunguzia mzigo wa gharama za matibabu.