Mmoja afariki dunia, wawili walazwa kwa kipindupindu Buchosa

Muktasari:

Wananchi wa Halmashauri ya Buchosa wametakiwa kufuata kanuni za afya ili kuepuka kupatwa na ugonjwa na kipindupindu, baada ya kubainika kuwepo kwa watu walioambukizwa.

Buchosa. Mtu mmoja amefariki na wawili wakilazwa kwa ugonjwa wa kipindupindu ulioikumba  Halmashauri ya Buchosa mkoani  Mwanza.

Awali ugonjwa huo ulisababisha  vifo vya watu watatu wilayani Sengerema wakiwa miongoni wa watu 74 walioambukizwa. 

Taarifa iliyotolewa leo Februari 8, 2024  na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa, Idama Kibanzi kwenye kikao ya baraza la madiwani cha halmashauri hiyo kilichokuwa kikijadili na kupisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2024/2025, imesema watu wawili wamelazwa katika vituo vya afya Kome na Lugasa Kata ya Nyakaliro.

Amewataka madiwani na wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo ambao unasambaa na kuenea kwa kasi.

Kibanzi amesema wagonjwa hao wamepatikana kwenye kambi ya uvuvi ya mchangani Kata ya Buhama kisiwani Kome na Kata ya Bukokwa ambapo timu ya wataalamu imeweka kambi huko ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya kujikinga.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Buchosa, David Mndeba amesema yeye na timu yake wako kwenye maeneo husika wakitoa elimu ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.